NA MWANDISHI WETU, KILIMANJARO
MWENYEKITI wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema wabunge 19 waliofukuzwa uanachama Chadema wapo bungeni wakiwakilisha familia zao na hawawakilishi wanawake wa Chadema.
Mbowe ameyasema hayo leo Jumatano, Machi 08, 2023 kwenye kongamano la Wanawake wa Chadema (Bawacha) lililofanyika mkoani hapa na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alimwambia Rais Samia kuwa Bawacha wana maumivu makubwa kwa kuona bungeni wapo wanawake ambao hawakwenda kwa kufuata taratibu za chama bali waliingia Bungeni kwa njia ovu kwa baraka ya Bunge na Taasisi nyingine za Serikali.
Mheshimiwa Rais, najua unafahamu kuwa hakuna zuio lolote linalomkaba Spika asiwaondoe bungeni wabunge wale 19. Na tunajua wewe ndio unaoidhinisha mishahara yao. Tunaomba wabunge wale waondolewe bungeni ili kuokoa pesa za walipata kodi zinazotumika kuwalipa mishahara. Wabunge wale hawawakilishi wanawake wa Chadema kama ilivyotakiwa, wale wanawakilisha familia zao. Tunataka waondolewe bungeni” alisema Mbowe