NA MWANDISHI WETU, RUVUMA
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe ameielekeza Serikali kusimamia madai ya wakulima ambao hawajalipwa fedha zao tangu 2020 baada ya mahindi yao yenye thamani ya zaidi ya sh. Biln sita kukusanywa na mfanyabiashara ambaye hadi sasa hajafanya malipo.
Wakulima hao 1008 wanadaiwa kukusanya mahindi yao kwa mfanyabiashara aliyefahamika kwa jina la Christopher Njako ambaye baada ya kuchukua mahindi hayo aliahidi kulipa kwa wakati lakini hadi sasa utekelezaji haujafanyika.
Zitto aliyasema hayo Mei 28, 2023 kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho ambao ukifanyika katika viwanja vya Tamasha mjini Peramiho Mkoani Ruvuma.
Kwa mujibu wa Kiongozi huyo mfanyabiashara huyo aliwahi kukamatwa na baadaye akaachiwa na hadi sasa hajafanikisha kuwalipa wakulima hao .
” Serikali ihakikishe wakulima wanalipwa fedha zao kuondoa sintofahamu iliyopo kwasasa kutokana na kutopata haki yao baada ya mahindi yao kuchukuliwa na mfanyabiashara huyo” alisema.
Wakulima hao wa Mahindi kutoka mikoa mbalimbali katika soko la Mkako Wilaya ya Mbinga Vijijini wanadaiwa kukusanya magunia ya mahindi 84,302.
Inadaiwa kuwa baada ya kuona kimya waliandika barua yao ya malalamiko mwaka 2020 kwa Ofisi ya Naibu Waziri wa Kilimo wakielezea madai yao na kuiomba Wizara kuwasaidia kupata fedha zao.
Ofisi ya Naibu Waziri wa Kilimo ilijibu barua hiyo Desemba 18 , 2020 ikikiri kupokea barua kutoka kwa Umoja wa wakulima wa mahindi na kuahidi kufanyia kazi suala hilo.

Hata hivyo 2021 baada ya ukimya kwa kutopata haki zao wakulima hao waliandika barua nyingine kwa Rais wakifikisha malalamiko yao baada ya mfabyabiashara huyo kukwama kuwalipa fedha zao tangu alipochukua mahindi yao.
Waziri Kivuli wa Biashara ACT Wazalendo Halima Nabalang’anya alitaka Serikali ifanye mchakato wa uwekezaji wa Viwanda hususani eneo la mahindi ili kuliongezea thamani zao hilo.
Alisema kwasasa zipo mashine za kukoboa na kusafa pekee na endapo viwanda vitajengwa katika mkoa wa Ruvuma ambao unaongoza katika uzalishaji wa mahindi itasaidia pia kutoa ajira kwa vijana.
Alisema bodi ya mazao mchanganyiko pia inatakiwa kununua mazao kwa faida ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wakulima.
Waziri Kivuli wa fedha w ACT Wazalendo, Emanuel Mvula kwa upande wake alieleza kuwa tokea mikutano ya chama hicho ilipotangazwa mkoani humo kumekuwa na jitihada mbali mbali za kuhujumu ikiwa ni pamoja na bendera za Chama hicho kuibwa