NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke kupitia Operesheni ya ukaguzi pamoja na kuangalia miundombinu yake wamefanikiwa kumkamata Jimmy Amani mmiliki wa kampuni ya Royal Recycling Limited kwa tuhuma ya kutumia umeme bila mita jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Kampuni hiyo ya Royal Recycling Limited inanzalisha mifuko ya Plastic inayopatikana Kata ya Kurasini, Mtaa wa Tumbaku Klabu ambapo TANESCO Mkoa wa Temeke walikuwa wanaendelea na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam akiwa Operesheni ya ukaguzi pamoja na kuangalia miundombinu katika Kata ya Kurasini, Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke, Mhandisi Jahulula Jahulula, amesema kuwa mmiliki wa Kampuni ya Royal Recycling Limited Amani wamemkuta anatumia umeme wa TANESCO asilimia 100 bila kutumia mita.
Mhandisi, Jahulula alisema kuwa utaratibu wa kumchukulia hatua unaendelea ikiwemo kumkatia umeme pamoja na kukamatwa na vyombo vya dola kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mhandisi Jahulula ameeleza kuwa Operesheni hiyo ni endelevu na sehemu ya majukumu yao ya kila siku katika kuhakikisha wanawatembelea wateja ili kutatua changamoto pamoja na kukagua miundombinu ya TANESCO.
Aidha Ofisa Usalama Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Stephen Maganga, alisema kuwa wizi wa umeme unarudisha nyuma jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassani katika kutoa huduma kwa wananchi kupitia TANESCO.
Maganga alisema kuwa mtu akitumia umeme bila kulipa mapato ya Shirika yanapotea, huku akitoa wito kwa watanzania kuwa wateja wenye uweledi ili jitihadi za kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya umeme inafikiwa.
Mhandisi kutoka Kanda ya Mashariki, Mrisho Sangiwa, amesema kuwa kutumia umeme bila kufata utaratibu ni hatari kubwa ambayo ingeweza kusababisha moto katika eneo hilo.
“Mteja wetu aliunga wire kwenda katika mashine za kuzalisha bidhaa zake bila kufata utaratibu hivyo usalama mali pamoja na binadamu ulikuwa katika mashaka makubwa” amesema Mhandisi Sangiwa.
TANESCO Mkoa wa Temeke wamejipanga kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake sambamba na kuwasaka wateja wote wanao hujumu miundombinu yake ya umeme.