NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete,amesema watumishi wa umma wazembe na wasiowajibika hawatakuwa na nafasi katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo Desemba 12, 2025 jijini Dar es Salaam katika mkutano na Waandishi wa Habari, Waziri Ridhiwani amesema tabia ya watumishi kufanya kazi kwa mazoea imefika mwisho.
Amesisitiza kuwa wakati huu si wa “kucheza-cheza” kazini, bali ni kutekeleza majukumu kwa maslahi ya umma kwa weledi na uadilifu.
Amesema endapo kuna jukumu lisilowezekana kutekelezwa ndani ya muda uliowekwa, mtumishi anapaswa kuwa muwazi na kutoa taarifa mapema badala ya kukubali halafu akashindwa kulitekeleza.
“Nataka kusema wazi, sitawavumilia watumishi wa umma wenye nidhamu ya uwoga. Kama jambo haliwezekani, sema mapema. Si kukubali halafu baadaye kushindwa na kuanza kutoa visingizio,” amesema.
Ameongeza kuwa mabadiliko katika utumishi wa umma ni lazima na yatafanyika bila kusita.
“Watumishi wa umma wazembe mnaowataka kuwaona vijiweni hivi karibuni mtawaona.
Kama kuna mtu ana shaka na kauli hizi ajaribu tu. Sitakubali mtu kuomba radhi kwa niaba ya mtumishi aliyekosea. Akikosea, amekosea na tutachukua hatua,” amesema, akisisitiza kuwa watumishi wanapaswa kuwa na adabu na uwajibikaji.
Katika hatua nyingine, Waziri Ridhiwani amesema wizara yake inakamilisha muswada wa sheria utakaowapa mamlaka ya kuwawajibisha watumishi wa ngazi ya chini wanaojihusisha na vitendo vya rushwa. Hatua hiyo inatokana na agizo la Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, la Desemba 11, 2025 kuhusu kufanya mapitio ya sheria ili kuhakikisha kundi hilo la watumishi nalo linawajibika ipasavyo.
Ameeleza kuwa sheria ya sasa haina vifungu vinavyowagusa moja kwa moja watumishi wa ngazi za chini, hivyo muswada mpya utapanga makundi ya watumishi kulingana na nafasi zao ili kuwezesha uwajibikaji kwa haki na kwa usahihi.
Aidha, Waziri Ridhiwani amesema serikali itaendelea kuhakikisha mchakato wa upatikanaji wa ajira katika idara, taasisi na mashirika ya umma unafanyika kwa uwazi na kwa kuzingatia misingi ya ushindani kama inavyoelekezwa na sera ya ajira nchini.
Amebainisha kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, serikali imetoa vibali vya ajira 41,500, ikiwemo nafasi 12,000 ambazo ni miongoni mwa ahadi za Rais Samia Suluhu Hassan. Kati ya nafasi hizo, 5,000 ni kwa kada ya afya na 7,000 kwa kada ya uwalimu wa masomo ya sayansi na hisabati.
“Ajira 12,000 tayari zimetangazwa na usaili unaanza kesho. Usaili utafanyika katika kila mkoa, hivyo hakuna sababu ya mtu kusafiri kuja Dar es Salaam. Usaili wa awali utafanyika kwa mfumo wa kielektroniki. Watakaofanikiwa kuitwa kwenye usaili wa ana kwa ana wanapaswa kufika wakiwa na vyeti vyao halisi,” amesema.






