NA MWANDISHI WETU, IRINGA
NAIBU Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe amesema serikali itahakikisha kiwanda cha maziwa cha Njombe kinafufuliwa kwa haraka ili kuleta manufaa kwa wafugaji na wanahisa.
Alisema hayo akijibu swali la msingi la Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Mwanyika (CCM) aliyetaka kujua mpango wa serikali wa kufufua kiwanda hicho.
Akijibu, Kigahe alisema serikali inatambua changamoto za kiwanda hicho. Alisema serikali kupitia uongozi wa mkoa imekwishaanza kuchukua hatua za kukwamua kiwanda hicho.
Alitaja hatua za awali zilizochukuliwa ni pamoja na kukutanisha wanahisa wa kiwanda na uongozi wa Mkoa wa Njombe.
“Aidha, napenda kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kuwa, kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Njombe, serikali itahakikisha kiwanda hicho kinafufuliwa kwa haraka ili sekta ya viwanda vya maziwa izidi kukua na kuleta manufaa kwa wafugaji na wanahisa,” alisema.