NA DENIS SINKONDE, SONGWE
SIKU kadhaa baada ya Waziri wa Maji Juma Aweso kumuagiza Meneja wa Wakala wa maji na Usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Charles Pambe, kufuata taratibu za kisheria kuvunja mkataba na Mkandarasi Helpdesk wa Jijini Dar es salaam anayetekeleza mradi wa maji Itumba-Isongole, Wilaya ya Ileje mkandarasi huyo amekaidi na ameendelea kutekeleza mradi huo.
Katibu Tawala mkoa wa Songwe Happiness Seneda amesikitishwa na hatua za mkandarasi huyo kukaidi agizo la waziri Aweso la kumwondoa kwenye mradi huo lakini bado anaendelea na kazi ya kupeleka mabomba kwenye mradi bila mkataba.
Seneda amesema hayo Mei 9,2023 akiwa kwenye ukaguzi wa miradi wilayani Ileje na kumkuta msaidizi wa mkandarasi akiwa kwenye mabomba aliyoweka barabarani tayari kupeleka kwenye mradi hali iliyomfanya kumsitisha kuendelea na kazi
Akizungumza na mwakilikilishi wa mkandarasi huyo kutoka kampuni ya Helpdesk iliyokuwa ikitekeleza mradi huo amemwambia ni marufuku kuonekana kwenye mradi huo ,kwani serikai ipo kwenye mchakato wa kutafuta mkandarasi mwingine atakayetekeleza kwa wakati kupitia nguvu za wananchi.
“Najiuliza kiburi cha kukaidi agizo la mkuu wa mkoa ,waziri wewe ni mkandarasi wa aina gani unafanya kazi bila mkataba acha kudharau maagizo ya viongozi wa serikali”,amesema Seneda.
Seneda amesema mkandarasi huyo alipaswa kumaliza mkataba Machi 2023 kwa lengo la kutatua changamoto ya maji kwa wakazi was Itumba na Isongole wilayani ambapo serikali ilitoa bilioni 4.9 lakini hakuna alichokifanya kwani ametekeleza Kwa asilimia 20 pekee.
“Ni lini fedha za mradi huu zitaachwa kuchezewa acheni kabisa na sisi hatukutaki mkoani kwetu maana unachonganisha wananchi na serikali kwani fedha zipo uache ubabaishaji”, amesema Seneda.
Aprili 25,2023 waziri Aweso alitoa maagizo ya kuvunja mkataba na mkandarasi huyo baada ya kupokea kero kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dk.Francis Michael, juu ya kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi licha ya serikali kumpa fedha za awali kiasi cha shilingi bilioni 1.2.