NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na Shirika la Mahusiano ya Kimataifa la Ujerumani (GIZ) wamekubaliana kushirikiana kwenye uwezeshaji katika sekta ya biashara hususan eneo la wafanyabishara wanawake na vijana wanaovuka mipaka.
Aidha, eneo jingine la taasisi hizo mbili zimeonesha nia ya kushirikiana ni eneo muhimu la taarifa za biashara ili kurahisisha wafanyabiashara kuzipata kwa njia rahisi.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Ukuzaji Biashara wa TanTrade, Fortunatus Mhambe wakati akizungumza katika mkutano uliofanyika kwenye ofisi za TanTrade zilizopo Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Julius Nyerere.
Mhambe amesema kuwa uwezeshaji huo unalenga zaidi miradi ya maendeleo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo waliopo maeneo ya mipakani ili kuwarahisishia kufanya biashara kwa ufanisi, kukuza shughuli zao na uchumi kwa ujumla.
Pia amesema uwezeshaji huo unalenga kuwezesha kwenye ukusanyaji wa hatua za uingizaji na uuzaji wa mazao na bidhaa mbalimbali nje ya nchi kwenye mfumo wa Trade Information Portal.
Naye Meneja wa Mradi kutoka GIZ, Claudia Hofmann amesisitiza kuwa, nchi ya Ujerumani ipo tayari kuimarisha uhusiano wa kibiashara na Tanzania kwa kuwawezesha wafanyabiashara wadogo waliopo mpakani hususan wanawake na Vijana, hivyo wamekuja na mpango mkakati wa kuwasaidia kwa kuwajengea uwezo wa uhuru na ufanisi zaidi.
Claudia ameongeza kuwa “Programu hii inalenga kukuza biashara ndani na nje ya Tanzania hivyo tumejipanga kutoa mafunzo na kuwapa wadau wetu nafasi za kuonesha bidhaa zao, kuwajengea uwezo wa kufanya biashara kwa uhuru na ufanisi zaidi na pia tunatoa nafasi kwa wadau kupata masoko mbalimbali ndani na nje ya nchi”.