NA MWANDISHI WETU, BIHARAMULO
WIZARA ya Nishati imekamilisha mradi wa kupeleka umeme kwenye mgodi wa kuchimba dhahabu Stamigold Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, ambapo mgodi huo ulikuwa unatumia nishati ya mafuta katika shughuli zote za uendeshaji.
Meneja wa Tanesco Mkoa wa Kagera, Godlove Mathayo amesema kuwa tayari serikali imetumia kiasi cha Sh.Bilioni 15 kwa ajili ya kujenga kilometa 105 kutoka kituo cha kupokea umeme cha Mpovu kilichopo mkoani Geita.
Alisema kuwa mradi huo ulikamilika Aprili 20, mwaka huu na tayari mgodi huo unatumia umeme katika uendeshaji wa shughuli zake, ambapo kiasi cha Sh milioni 900 kitaokolewa kwa mwaka kutokana na kutoka hatua ya kutumia nishati ya mafuta mpaka nishati ya umeme.
Alisema njia ya umeme iliyojengwa ni ya ukubwa wa kilovoti 33 na ujenzi umehusisha njia ya kusafirisha umeme pamoja na kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Stamigold.
“Kituo kimejengwa kwa transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 10 kila moja, na transfoma mbili za MVA 2.5, tunaamini shughuli za mgodi zitaendelea vizuri na changamoto zitapungua, kwani matumizi ya umeme katika mgodi huu ni kilio cha muda mrefu, “alisema Mathayo.
Kufuatia upatikanaji wa umeme katika mgodi huo, Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Advera Bulimba ametoa wito kwa wawekezaji kuwekeza wilayani humo kutokana na uwepo umeme wa uhakika.
Alisema kwa sasa hakuna changamoto tena ya kuzimika kwa umeme mara kwa mara au mgawo kama miaka ya nyuma.