NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BARAKA Matamburo (30) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo akikabiliwa na shitaka la wizi wa Sh. 245,000, mali ya Grace Mwinuka.
Baraka alisomewa shtaka na karani, Emmy Mwansasu mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kariakoo, Claudis Kipande.
Akisoma hati ya mashtaka, Emmy alidai mbele ya mahakama kuwa kijana huyo anashtakiwa kuiba Aprili 26, mwaka huu saa 10:30 jioni katika eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili, Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam ambaye ni mlinzi hapo.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo. Mlalamikaji, Grace aliieleza mahakama atakuwa na shahidi mmoja katika kesi hiyo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 9, mwaka huu itakaporudi mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.
Mshtakiwa ataendelea kubaki rumande kwa kuwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na mdhamini mmoja atakayesaini bondi ya Sh. 200,000.
Wakati huohuo Mahakama ya Mwanzo Kariakoo imemuachia huru mkazi wa Kiwalani, Dar es Salaam, Rajabu Twaha (63) baada ya mlalamikaji kuiomba mahakama ifanye hivyo.
Rajabu alikuwa akikabiliwa na shtaka la shambulio la kumdhuru mwili mkazi wa Makongo, Mussa Juma (35). Mussa aliiomba mahakama iiondoe kesi hiyo kwa kuwa amemsamehe Rajabu kama baba yake.
Mussa alitoa ombi hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Claudis Kipande wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo.
Awali Karani wa Mahakama hiyo, Emmy Mwansasu alidai kuwa Mei Mosi, mwaka huu 2:30 usiku eneo la Ocean Road Wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam, Rajabu alimshambulia Mussa Juma kwa kumchoma na mkasi ubavuni upande wa kushoto.