NA MWANDISHI WETU, MWANZA
WATU wenye ulemavu wilayani Misungwi, mkoani hapa, wamepongeza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kupitisha mikopo ya makundi maalum Benki, badala ya halmashauri, hatua itakayorahisisha upatikanaji wake kwa walengwa.
Wameeleza furaha yao leo Mei 2, 2023 wakati wa hafla ya uhuishaji kamati za ulinzi kwa wenye ulemavu wilayani humo, iliyoandaliwa na Shirika la kimataifa la Sense, linaloshirikiana na Serikali ya Tanzania kuibua wenye ulemavu, ili kuwawezesha kutambua na kutumia fursa zilizomo katika maeneo yao, ikiwemo mikopo ya asilimia mbili.
Mmoja wa wenye ulemavu, Malimi Luhanya, amesema Benki ni sehemu sahihi kwasababu wanaotoa mikopo wana taaluma ya kutosha kwa masuala ya fedha, ambao watasaidia, pamoja na mambo mengine, kutoa elimu ya ujasiliamali, ili kuwainua kiuchumi na kurahisisha marejesho.
“Mchakato pia utafupishwa kwasababu Benki kazi yao ni kushughulika na fedha tu, tofauti na halmashauri ambapo wanaotuhudumia, ikiwemo maofisa ustawi, wanakua na majukumu mengine ya kiofisi na sio mikopo tu,” amesema.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wenye Ulemavu (Shivyawata) Misungwi, Jesca Bonaventura, amesema kutokana na wanaoshughulikia mikopo katika halmashauri kuwa na fani tofauti na masuala ya fedha, wenye ulemavu wanalazimika kutafuta wasaidizi wa kuwaelimisha michanganuo inayohitajika, kwa gharama.
“Kwahiyo hata kamati zilizohuishwa zitatupunguzia baadhi ya michakato katika masuala mengi, kwasababu zinaundwa na watu wenye taaluma mbalimbali, ambao jukumu lao ni kutusaidia,” amesema.