NA MWANDISHI WETU , ARUSHA
VUTA nikuvute imetanda jijini hapa kufuatia Mkuu wa wilaya ya Arusha Felician Mtehengerwa kusema kitendo cha wafanyabiashara wadogo (Machinga) katika jiji la Arusha kuandamana usiku kinachochewa na wanasiasa wenye nia ovu ya kuihujumu serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha DC huyo amemtuhumu Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo kuwa kinara wa mpango huo haramu kwa kisingizio cha kubughudhiwa na Mgambo wa Jiji.
Akizungumza na vyombo vya habari na kutoa ufafanuzi madai hayo ,Mtehengerwa alidai kuwa Jambo hilo linaratibiwa na kuchochewa na wanasiasa kwa lengo la kuichafua serikali na kuwachonganisha wafanyabiashara hao na serikali yao.
Alidai upo ushahidi kwamba Gambo amewapeleka baadhi ya viongozi wa machinga bungeni dodoma kwa lengo la kuwachongea viongozi wa mkoa ili waonekani hawafai kwa kisingizio cha migambo kutesa machinga kwa kipigo
Alimtaka Gambo kuacha siasa za maji taka kwani uongozi wote wa mkoa unajua jinsi anavyo hujumu kwa kutumia majukwaa ya kisiasa
“Jana usiku Machinga wameandamana katika katakana ya jiji la Arusha wakidai mwenzao Isaac Sangwa ameuawa kwa kupigo cha Migambo huu ni uzushi na ni mpango mchafu unaochochewa na wanasiasa wachache kwa maslahi yao ili kumhujumu rais Samia Suluhu ,wasitake kutulazimisha tutumie mamlaka yetu tulionayo “
Alisema wao kama viongozi hawawezi kuruhusu Machinga kufanya biashara kiholela wakati walishatengewa maeneo yao .
“Hili ni jiji la utalii hatuwezi kuruhusu Machinga afanyebiashara kiholela hii ni kufukuza watalii kwa sababu ya wanasiasa uchwara wanaoendesha siasa za maji taka kusaka umaarufu “
Awali wamachinga wa soko la Kilombero jijini hapa, waliandamana wakiwa na madai mbalimbali ya kunyanyaswa kwa kipigo,kuombwa rushwa ya ngono na pesa na Mgambo wa jiji la Arusha.
Jitihada za kumpata Gambo ili kuzungumzia tuhuma hizo hazikuzaa matunda.