NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MAJERUHI Osam Milanzi aliyeruhusiwa jana Machi 28, 2023 kutoka hospitali baada ya kugongwa na basi la mwendokasi februari 22 mwaka huu anatarajia kurejea hospitali baada ya wiki mbili kwa uangalizi zaidi
Hayo yamebainishwa na Meneja Uhusiano wa Taasisi ya Tiba na Mifupa ya Muhimbili (MOI), Patrick Mvungi leo Machi 29, 2023 jijini Dar es salaam ikiwa ni siku moja baada ya Milanzi kuruhusiwa kutoka hospitali
Mvungi amesema kuwa Milanzi anaendelea vizuri na anaweza kuzungumza japokuwa sio kila kitu.
“Ndugu yetu huyu ameruhusiwa jana na anaendelea vizuri na anaweza kuzungumza japokuwa sio kila kitu, Osam anatakiwa kurejea hospitali baada ya wiki mbili kwa uangalizi zaidi,” amesema
Hata hivyo katika taarifa kwa Umma, iliyotolewa jana na Mvungi amesema Milanzi ameruhusiwa kutoka hospitali baada ya afya yake kuimarika.
Amesema Milanzi alipokelewa MOI Februari 22, 2023 ambapo alipata huduma za kibingwa katika kitengo cha dharura (EMD), ICU, HDU na wodi 2A .
“Milanzi alipokelewa MOI akiwa ameumia maeneo ya kichwa, mguu wa kushoto, mkono na bega upande wa kulia, Milanzi ataendelea na huduma kama mgonjwa wa nje na atarudi kliniki baada ya wiki mbili,” amesema
Aidha, Mvungi alitoa shukran za dhati kwa watanzania wote, vyombo vya habari ambao kwa pamoja wameshirikiana nao katika kumuombea na kumtangaza Milanzi.