NDOLA, ZAMBIA
MWANAFUNZI wa shule ya Sekondari ya Bweni ya Mansa nchini hapa aliyefahamika kwa jina la Emmanuel Kayuni (21) amekutwa amefariki dunia eneo la Northrise, mjini Ndola katika nyumba ya mpenzi wake aliyetajwa kwa jina la Princess Mwaba .
Mauti ilimkuta Kayuni baada ya kudaiwa kutoroka shuleni ili kumtembelea mpenzi wake huku wazazi wakidhani kuwa kijana wao yupo shule akiendelea na masomo.
Kabla kifo chake,Inasemekana Kayuni alizirai baada ya kulalamika alikuwa akipata maumivu makali kwenye moyo.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa eneo hilo Peacewell Mweamba, tukio hilo limetokea Machi 22, 2023 na ripoti kutolewa kwa polisi na baba mzazi wa marehemu aliyefahamika kwa jina la John Kayuni.
“Taarifa fupi kuhusu suala hilo ni kuwa marehemu alikwenda shuleni kule Mansa mnamo Januari 2023 lakini akatoka shule kukutana na mpenzi wake Princess Mwaba mwenye umri wa miaka 20” Mweeba amesema
Amesema kuwa Kayuni alikuwa amerejea kutoka shule ya bweni na kujificha kutoka kwa wazazi wake ambao waliamini kuwa alikuwa bado yuko shulemi.
“Mnamo Machi 21, 2023, mwendazake na mpenzi wake walienda katika nyumba ya kulala wageni ya Executive kule Northrise ambako walilala na alikuwa analalamika kuhusu matatizo ya moyo. Asubuhi, wawili hao walitoka na kwenda katika nyumba yao ambako marehemu alimuacha mpenzi wake saa tatu asubuhi ili kununua nyanya sokoni,” mkuu wa polisi amesema.
Saa moja baadaye, Kayuni alizirai kwenye geti alipokuwa akirejea nyumbani kwa mpenzi wake huku mfanyakazi wa kutunza maua na mashamba eneo hilo akijaribu kumuhudumia.
Mpenzi wake alielezwa kilichotokea kwa Kayuni na kutafuta usafiri ili kumkimbiza hospitalini lakini akawa amefariki.
.