NAIROBI, KENYA
WAKENYA wametakiwa kutafuta mbadala wa mahindi baada ya nchi hiyo kukumbwa na uhaba wa chakula chake kikuu, kufuatia ukame wa muda mrefu.
Waziri wa Kilimo, Mithika Linturi amewaambia wabunge kwamba uhaba katika soko la dunia unafanya iwe vigumu kwa serikali kununua nafaka hiyo.
“Kwa hivyo ninawahimiza Wakenya kuegemea kwenye mchele, viazi na vyakula vingine mbadala. Tayari tumeleta tani za mchele na tunaleta zaidi wiki ijayo,” amesema Linturi.
Linturi amesema anamatumaini kuwa bei ya unga wa mahindi itapungua katika muda wa siku 10 zijazo wakati meli inayobeba tani za mahindi na mchele itakapotia nanga nchini humo.
Mfuko wa kilo 90 wa mahindi kwa sasa unauzwa kwa shilingi za Kenya 5,600 (sawa na sh.100,000 za Tanzania).
Hata hivyo maduka ya ndani nchini hapa yamedai huenda gharama itashuka wakati uagizaji huo utakapowasili.
Kupanda kwa gharama za maisha ikiwemo bei ghali ya mahindi nchini humo ndio kitovu cha maandamano ya upinzani yaliyoanza Jumatatu iliyopita.