NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI ya Tanzania na Japan zimekubaliana kuendeleza ushirikiano katika kutekeleza miradi ya Nishati.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alipokutana na kufanya mazunguzo na Balozi mpya wa Japan, Yasushi Misawa katika ofisi za Wizara ya Nishati mkoani Dodoma.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha na Ubalozi wa Japan nchini.
Katika mazungumzo hayo, Mramba ameishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati ukiwemo wa kuhamasisha matumizi ya Gesi Asilia.
Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Yasushi Misawa amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa amekuja Wizara ya Nishati ili kujitambulisha na kueleza kuwa Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali inayoendelea.
Amesema pia atatumia nafasi hiyo kuhamasisha matumizi ya Gesi Asilia, kuzalisha umeme kutokana na Nishati Jadidifu hasa Upepo na ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Ameongeza kuwa, Japan imeendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali katika Sekta ya Elimu, Afya, Maji, pamoja Ujenzi wa miundombinu.
Baadhi ya miradi ya umeme ambayo inatekelezwa kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili ni pamoja na njia ya kusafirisha umeme ya msongo mkubwa wa Kilovolti 400 katika mradi wa Backbone na vituo vya Kupoza na Kusambaza Umeme katika maeneo mbalimbali nchini.