NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI imejipanga vema kusimamia na kuendeleza michezo sita ya kipaumbele ya kimkakati ikiwemo mpira wa kikapu ili kuleta tija katika sekta ya michezo nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Saidi Yakubu amesema hayo Machi 9, 2023 Ofisini kwake Mji wa Serikali jijini Dodoma katika kikao chake na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini Michael Kadebe alipofika kujitambulisha kwa Katibu Mkuu huyo baada ya kuteuliwa na Rais Dk Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.
“Nguvu yetu kwa sasa tunaelekeza kwenye miundombinu ya michezo, maeneo ya mazoezi na kupumzikia katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma, kukarabati uwanja wa Benjamin Mkapa pamoja na sports arena Dar es Salaam itakayokuwa na uwezo wa kuingia watu 15,000 na Dodoma itakayokuwa na uwezo wa kuingia watu 16,000” amesema Yakubu.
Michezo hiyo ya kipaumbele ni mpira wa miguu, netiboli, mpira wa kikapu, riadha, ngumi na mchezo wa kuogelea.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini Kadebe amesema shirikisho hilo linaratibu mashindano ligi ya mchezo huo kwa mikoa yote nchini na hatimaye kuwa na bingwa wa kitaifa kwa mchezo huo.
Aidha, Kadebe pia amemtembelea Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nicholous Mkapa na kujitambulisha kwake.