NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya Weka Jiji Safi (WEJISA Company Ltd) kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wake Nuru Hassan imepongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuweka mazingira mazuri ya kufanya kazi ikiwemo wafanyakazi Wanawake, jambo ambalo limeongeza uchapakazi kwa jinsia hiyo.
Nuru amesema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani Machi 8 , 2023.
“Rais wetu Samia tunamuunga mkono kwa sababu nafasi aliyonayo amesaidia kuongeza mwamko kwa wanawake kufanya kazi na wale ambao walikua hawana kazi na kutafuta shughuli zozote ili waweze kujiondoa kwenye utegemezi,” amesema Nuru.
Amesema kuwa, kampuni ya WEJISA itaendelea kushirikiana na Serikali bega kwa bega na ndio maana leo wamekwenda kusheherekea pamoja na kujifunza mengi kwa wafanyakazi wao wa kike
Aidha, amesema kuwa amepata faraja kujumuika na wanawake hao kwani wamekuwa chachu ya maendeleo ya Kampuni hiyo.
Wanawake hao wa WEJISA wanatoka vitengo mbalimbali ikiwemo wanaosafisha maeneo ya Jiji, ufagiaji, ukusanyaji wa taka na usafi wa mazingira.
Lengo la tukio hilo ni kupeana moyo kama wanawake katika kuamua mambo katika kufanikisha utendaji bora wa kazi.
Kwa upande wake Patricia Kimelemeta Mwandishi Kinara wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto Mkoa wa Dar es Salaam ametoa mada ya malezi na makuzi kwa watoto katika tukio hilo la kusheherekea siku ya wanawake, ambapo alitoa raia Kwa wazazi kuendelea kutoa elimu kwa watoto wao ikiwemo kujenga ukaribu wa kuwachunguza ili kujua changamoto wanazokutana nazo.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wanawake wafanyakazi wa WEJISA wameishukuru kampuni hiyo kwani imekuwa mkombozi kwao na wamekuwa wakifanya kazi moyo.
Aidha, amewataka wanawake kuzingatia sheria za usalama barabarani kwani wamekuwa wakishuhudia matukio mengi, ikiwemo wao kugongwa.
Kwa upande wake Sharifa Magombeka amesema kuwa, anafanya kazi ya kuzoa taka ili kupata kipato chake halali,
“Mwanamke ni kujitambua, nafanya kazi yangu ya kuzoa taka hii kupata kipato kihalali, tunamshuru Rais kuendelea kueka mazingira ya ufanyaji kazi,
leo tumejumuika hapa tumepata elimu, lakini pia tumefuraia pamoja” amesema Magombeka