NA MWANDISHI MAALUM, DOHA
SERIKALI ya Estonia imeahidi kuisaidia Tanzania kuboresha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya ukusanyaji kodi ili kusaidia kupiga hatua zaidi katika masuala ya usimazi wa kodi na kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Masuala ya Uchumi na Maendeleo wa Estonia, Marjin Ratnik, alipofanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk.Mwigulu Nchemba mjini Doha, Qatar, kando ya Mkutano wa Tano wa Umoja wa Mataifa wa nchi zinazoendelea za kipato cha chini unaoendelea nchini humo.
Ratnik amesema Serikali yake ipo tayari kuwapokea wataalamu kutoka Tanzania kupata mafunzo ya mifumo ya tehama ya ukusanyaji kodi nchini humo kwa vitendo ili wapate utaalam utakaowasaidia wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Dk Nchemba, amesema Serikali imepokea rasmi mwaliko wa kuwapeleka wataalamu wa Tanzania kupata mafunzo hivyo wameanza maandalizi ya safari hiyo ambapo mwezi Mei mwaka huu wataalam wanaohusika na masuala ya ukusanyaji kodi watakwenda nchini Estonia kujifunza mifumo mbalimbali ya ukusanyaji kodi.
“Juhudi hizi ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan, la kuboresha mifumo ya kodi ili kuwepo na uwazi katika ukusanyaji”amesema Dk. Mwigulu.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Saada Mkuya amesema kuwa kuwepo kwa mifumo bora ya ukusanyaji kodi itaongeza uwajibikaji wa watalaam wanaohusika na ukusanyaji kodi.
Ameongeza pia kuwepo kwa mifumo ya pamoja ya ukusanyaji kodi itamsaidia mlipakodi kulipa kodi mara moja katika Taasisi zote zinazohitaji kufanya hivyo.
Katika tukio jingine Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa wa Ufaransa, Chrysoula Zacharopoulou ambapo Waziri huyo amesema Serikali yake ipo tayari kusaidiana na Tanzania katika ujenzi wa bandari itakayohudumia Tanzania na nchi jirani
“Ufaransa ipo tayari pia kutusaidia kukuza sekta binafsi ambayo imekuwa ikitoa ajira nyingi kwa vijana nchini”, amesema Dk. Nchemba.
Ameongeza kuwa Serikali ya Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuboresha miundombinu ya barabara, nishati na umeme wa jua ili iweze kutumika katika shughuli za uzajilishaji.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Saada Mkuya , amesema kuwa Ufaransa imetangaza rasmi kushirikiana na Tanzania katika kukuza sekta ya utalii kwa kuwa ina mchango katika pato la Taifa.
Ameongeza kuwa Serikali ya Ufaransa imekuwa ikiisaidia Zanzibar katika kuboresha sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, afya na nishati.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa wa Ufaransa Zacharopoulou, amesema kuwa pamoja na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ufaransa, anaamini kuwa bado kuna mengi zaidi ya kushirikiana kati ya nchi hizo mbili.
Zacharopoulou amepongeza msimamo wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia kwenye masuala ya jinsia na nia ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Jukwaa la Usawa wa Kizazi (Generation Equality Forum) baadaye mwaka huu.