NA MWANDISHI WETU, KILIMANJARO
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimempa Tuzo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Haasan.
Tuzo hiyo imetolewa na Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) leo Jumatano, Machi 08, 2023 kwenye kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lililoandaliwa na Baraza hilo ikiwa ni tuzo ya kuboresha na kuimarisha Amani nchini.
Wakati wakikabidhi tuzo hiyo, Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge amesema baraza lao limeona juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Samia za kuliunganisha taifa na kuondoa uhasama uliokuwapo kwa miaka sita iliyopita.
Pia baraza hilo limempa tuzo ya kuongoza maridhiano Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Bawacha wamesema Mbowe anastahili tuzo hiyo kwani pamoja na kubezwa kuwa amelamba asali lakini hakukata tamaa na matokeo yake ni maridhiano yaliyopatikana hadi leo Rais wa nchi ambaye ni Mwenyekiti wa chama tawala (CCM) amekubali kuhudhuria tamasha la chama cha upinzani.
Awali wakati akimkaribisha Rais Samia ambaye alikuwa ni mgeni rasmi kwenye kongamano hilo, Mwenyekiti wa Bawacha mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kihwelu amesema anayo furaha kuzungumza kwenye kongamano la Bawacha huku akiwa hana hofu ya kukamatwa na polisi wala kupigwa mabomu ya machozi.
Huko nyuma tulikuwa tunafanya makongamano haya tukiwa na hofu kubwa ya kuvamiwa na jeshi la Polisi, kukamatwa, kuumizwa, kupigwa mabomu ya machozi ili tamasha livunjike. Leo tupo hapa na Mheshimiwa Rais tukiwa hatuna tena hofu hiyo,” alisema Grace
Naye Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge, amempongeza Rais Samia kwa uungana nao kwani kutamsaidia kusikia maneno ambayo wanawake wa chama chake wa hawawezi kumwambia.
Mheshimiwa Rais, leo utayasikia matatizo ya wanawake wa Tanzania kutoka kwetu kwani tuna imani wanawake wa chama chako cha CCM huishia kukwambia unaupiga mwingi. Sisi tutakwambia ukweli na yale ambayo huwezi kuyasikia kwenye chama chako,” alisema Catherine Ruge
Kongamano la Bawacha hufanyika kila mwaka Machi 08 kwa kubadilisha mikoa. Mwaka jana kongamano kama hilo lilifanyika mkoani Iringa.