NA MWANDISHI WETU, DODOMA
WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Balozi Dk Pindi Chana amewasisitiza Wajumbe wa Menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufikia malengo ya Serikali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Said Yakubu akijadiliana jambo ma Waziri wa Wizara hiyo Dk Pindi Chana
Waziri Balozi Dk Chana amesema hayo Februari 28, 2023 wakati wa mapokezi ya Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Nicholas Merinyo Mkapa katika Ofisi za Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Februari 27, 2023 Ikulu Chamwino Dodoma.
Akizungumza na Menejimenti ya Wizara hiyo Waziri Balozi Dk Pindi Chana amewasisitiza viongozi wafanye kazi kwa ushirikiano ili kutekeleza malengo ya Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Tuna kazi ya kufanya, tufunge mkanda, timu imekamilika, nimesimama hapa tukumbushane habari ya “Team Work” Maana huku tayari tunaye Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu. Hawa wenzetu ni wataalam wa kufuatilia masuala tuliyopanga na kukubaliana kuyafanya” amesema Waziri Balozi Dk Chana.
Amewataka Wajumbe wa Menejimenti ya Wizara hiyo wampe ushirikiano wa kutosha Naibu Waziri mpya Mhe. Hamis Mwinjuma kama wanavyoendelea kumpa yeye ushirikiano katika kutekeleza majukumu yake.
“Tuna dhamana mbele ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna mambo ya kuonesha umma, uwezo tunao na nia ya kufikisha malengo ya Serikali ambayo tumepewa tunayo na sababu tunazo na tunawajibu wa kuhakikisha mambo yaende na yakamilike” amesisitiza Waziri Balozi Dk Chana.
Amesema kuwa wadau wa Wizara hiyo ni watu wote ambao wanaguswa kwa namna moja au nyingine kwenye sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ni wengi na wapo mikoa yote 26 kuanzia watoto, watu wazima, wanawake kwa wanaume na sekta hizo zinatoa ajira kwa wadau hao na kuongeza Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja kutokana na kazi wanazofanya.
Kwa upande wake Naibu Waziri Hamis Mwinjuma amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa dhamana aliyompa katika Wizara hiyo na kuwahakikishia menejimenti na watumishi wa Wizara hiyo kuwapa ushirikiano na kufanya kazi kama timu moja ili kufikia malengo ya yaliyowekwa.
“Mimi sitaki kushindwa, mambo yote ambayo tulikuwa tunayafanya kwa kushirikiana na BASATA, COSOTA, Bodi ya Filamu tutayaendeleza. Ninaomba ushirikiano wa kila namna, twende mpaka nje ya njia zetu wakati mwingine ili kuhakikisha mambo yanatimia” amesema Naibu Waziri Mwinjuma.
Ameongeza kuwa Wizara hiyo inapaswa kufanya kazi yake ya kutangaza na kuzisaidia wizara nyingine na jukumu la Wizara hiyo ni kulitangaza Taifa kwa usahihi zaidi kwa kushirikiana na Wizara zote hapa nchini.
Naye Katibu Mkuu Said Yakubu amesema kuwa Naibu Waziri Mwinjuma amekuwa mdau muhimu wa Wizara hiyo kwa muda mrefu na ameongeza nguvu katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara hiyo huku Naibu Katibu Mkuu Nicholas Mkapa akiwaomba ushirikiano wajumbe hao wa Menejimenti katika utekelezaji wa majukumu yake.