NA MWANDISHI WETU
ALIYEKUWA Mbunge wa JImbo la Arusha mjini, Godbless Lema leo Jumanne, Februari 28, 2023 ameondoka nchini Canada akirejea Tanzania.
Mwenyekiti huyo wa Kanda ya Kaskazini wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kesho Jumatano, Machi 1 Saa 5.30 asubuhi.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema atapokelewa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama chake pamoja na wanachama na moja kwa moja wataelekea kwenye mkutano wa hadhara ulioandaliwa jimboni kwake Arusha Mjini.
Lema aliondoka Tanzania Novemba, 2020 na kukimbilia Kenya akidai ametishiwa kuuawa. Alikaa Kenya kwa siku kadhaa kabla ya Desemba 10, 2020 kuondoka na kuelekea Canada alipopata hifadhi ya kisiasa yeye pamoja na familia yake.
Ujio wa Lema ni muendelezo wa viongozi wa Chadema waliokimbia nchi kwa sababu za kisiasa.Wengine waliorejea Tanzania baada ya kukimbia ni pamoja na Tundu Lissu na Hezekiah Wenje.