NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
VIJANA wamehamasishwa kuchangamkia fursa zilizopo katika miradi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuchangamkia fursa za uwepo wa miradi ya usambazaji umeme maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji kwa kuanzisha biashara na shughuli za kuwaletea maendeleo.
Rai hiyo imetolewa Juni 4, 2026 na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali (Mstaafu), Jacob Kingu alipotembelea banda la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti Kingu akiwa ameongozana na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy walipata maelezo juu ya miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA ikiwamo miradi ya nishati safi ya kupikia pamoja na miradi inayoendelea ya kufikisha umeme katika Vitongoji.
“Tumepata nafasi kutembelea Viwanja vya Sabasaba ambapo mwaka huu Maonesho haya yanatimiza miaka 50. Nafurahi kwamba Wakala wa Nishati Vijijini (REA) nao ni sehemu ya Taasisi zinazoonyesha biadhaa zake na huduma inazotoa.
Nawaomba wananchi waweze kufika kwenye maonesho haya na waweze kufika kwenye banda la REA ili waweze kuzijua fursa zilizopo katika miradi inayotekelezwa na REA kama miradi ya nishati safi ya kupikia ambapo vijana wanaweza kupata fursa ya kutenegeneza majiko banifu au mkaa mbadala,” amesema Mwenyekiti Kingu.
Ameongeza kuwa, uwepo wa umeme vijijini umekuwa ni chachu ya kukuza biashara na ajira kwa vijana na wanawake.

