NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amewataka wafanyabiashara wa Tanzania kutumia huduma za Ubalozi wa Tanzania nchini China wanapokusudia kufanya biashara au kuagiza bidhaa kutoka nchini humo ili kupata taarifa sahihi, kujenga mahusiano ya kuaminika na washirika wa biashara na kujiepusha na changamoto za utapeli.
Londo aliyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika Kliniki ya Biashara na Uwekezaji iliyoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Maalum Tanzania (TISEZA) kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini China, iliyofanyika katika viwanja vya Moaneshoy a 50 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba.
Kliniki hiyo imefanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo wafanyabiashara kuhusu namna salama ya kufanya biashara na kuagiza bidhaa kutoka China, sambamba na kuwatambulisha fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo nchini humo.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini China, Dk.Suleiman Suleiman, aliwahimiza Watanzania kuchangamkia fursa ya kuuza bidhaa katika soko la China kupitia utaratibu unaoruhusu bidhaa za Afrika zinazoafiki vigezo husika kuingia katika soko hilo bila ushuru.
Alisema hatua hiyo inatoa fursa kubwa kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa Tanzania kupanua masoko yao, kuongeza mauzo na kunufaika na soko kubwa la China.
Naye Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji wa TISEZA, George Mukono, alisema taasisi hiyo inaendelea kutekeleza jukumu lake la kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, kuhamasisha Watanzania kuwekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji na kuwaunganisha na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya ubia na ushirikiano wa kibiashara.
Alisema serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara, kuwafungulia fursa mpya za biashara na kuwaunga mkono wanapokumbana na changamoto katika shughuli zao za biashara ndani na nje ya nchi.

