NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
TANZANIA imeendelea kunadi fursa zake za uwekezaji katika maeneo maalum ya kiuchumi na maeneo ya uzalishaji kwa ajili ya mauzo nje ya nchi , huku ikilenga kuvutia wawekezaji kutoka Angola na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Hatua hiyo ilijitokeza wakati Mamlaka ya Uwekezaji na Kanda Maalum za Kiuchumi Tanzania (TISEZA) iliposhiriki Mkutano wa Siku ya Angola uliofanyika katika viwanja vya Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Mkutano huo, uliokuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Angola katika maonesho hayo, uliwakutanisha viongozi wa serikali, wanadiplomasia na wadau wa biashara kutoka Tanzania na Angola kwa lengo la kujadili namna ya kupanua biashara, uwekezaji na ushirikiano wa viwanda.
Akizungumza katika mkutano huo, Balozi wa Angola nchini Tanzania, Domingos De Almeida Da Silva Coelho, alisema nchi hizo mbili zina historia ya muda mrefu ya ushirikiano, lakini sasa kuna haja ya kuugeuza urafiki huo kuwa matokeo halisi ya kiuchumi.
“Angola na Tanzania zina uhusiano wa muda mrefu wa kirafiki, lakini kipaumbele kwa sasa ni kuugeuza urafiki huo kuwa ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji unaozalisha ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema.
Aliongeza kuwa majukwaa ya kimataifa kama Maonesho ya Sabasaba yana mchango mkubwa katika kuwaunganisha wawekezaji na kufungua fursa mpya za biashara.
“Haya si maonesho ya bidhaa pekee, bali ni jukwaa la kujenga madaraja ya kudumu ya kiuchumi kati ya mataifa yetu mawili,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi wa Uwekezaji wa TISEZA, Vedasto Kagombora, alisema Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kupitia mageuzi ya sera na mifumo ya udhibiti ili kuvutia na kuhifadhi wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.
Alisema Serikali imeweka mfumo thabiti na unaotabirika wa uwekezaji unaolenga kuongeza ushindani na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tunaendelea kufanya maboresho yanayolenga kuongeza ufanisi, uwazi na kupunguza urasimu ili wawekezaji wanaochagua Tanzania wanufaike na mazingira bora ya kufanya biashara,” alisema.
Washiriki wa mkutano huo walisisitiza kuwa kuna fursa kubwa za kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Angola katika sekta za kilimo, nishati, usafirishaji na viwanda, wakieleza kuwa ushirikiano wa kikanda ni muhimu katika kufanikisha mageuzi ya uchumi wa Afrika kwa muda mrefu.
TISEZA ilisema ushiriki wake katika mkutano huo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuitangaza Tanzania kama kitovu cha ushindani wa uwekezaji na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa unaochochea ukuaji jumuishi na endelevu wa uchumi.

