NA MWANDISHI WETU,MAKETE,NJOMBE
MAHAKAMA ya Wilaya ya Makete mkoani Njombe imewahukumu kulipa faini ya Sh.500,000 kila mmoja Maofisa Misitu Wawili wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) wa Halmashauri hiyo kwa
kosa la kuomba na kupokea rushwa Kinyume na kifungu cha 15(1)(a) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 R:E 2024.
Katika shauri hilo la jinai namba 8088/2026 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Makete Irvan Msacky dhidi ya Maofisa Misitu hao
Thadeus Mtui na Florian Kilango
sambamba na adhabu ya awali pia wameamriwa kurejesha kiasi cha Sh. Millioni nane kwa mfugaji Yuda Male ndani ya miezi miwili kuanzia tarehe ya hukumu kupitia ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa( Takukuru)wilayani hapa.
Wakati huo huo,Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Mkoa wa Njombe Daniel Mono ameieleza Mahakama kuwa washtakiwa waliomba na kupokea rushwa kiasi cha Sh 8,000,000/- kutoka kwa mfugaji Male (kwa nyakati tofauti), ili wasimchukulie hatua kwa kosa la kukutwa akichunga ng’ombe katika Hifadhi ya Msitu ya Chimala iliyopo wilayani Makete.
Washtakiwa wamesomewa hati ya mashtaka na kukiri kutenda kosa hilo na wote wawili wamelipa faini hiyo.

