NA JANETH JOVIN, MEATU
RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa wananchi wa Meatu na maeneo mengine nchini kuendelea kuzalisha pamba na mazao mengine ili kuendelea kusambaza mali ghafi inayohitajika kwenye viwanda na kuvutia uwekezaji
wa viwanda vingine.
Huku akiwapongeza wakulima wa Meatu kwa juhudi walizofanya, ambazo amesema zimeongeza uzalishaji wa pamba katika Halmashauri ya Meatu kutoka kilo 22,000,713 mwezi Novemba 2020 hadi kufikia kilo 40,286,000 kwa mwaka huu wa 2025.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Juni 17,2025 alipokuwa akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa stendi ya mabasi Meatu, mkoani Simiyu.
Rais Samia amesema wilaya hiyo imeendelea kushuhudia maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya ,Kilimo pamoja na Elimu.
Akizungumzia Kiwanda cha kuchakata pamba cha Biosustain Tanzania Limited ambacho amekizindua alisema wawekezaji wa kiwanda hicho waamekusudia kupanua uwekezaji wao kwa kuongeza kiwanda kingine chenye thamani ya Bilioni 12 kwaajili ya uzalishaji wa mafuta ya pamba na Alizeti.
Alisema hayo ni maendeleo makubwa kwa nchi,hivyo amewahamasisha kufanya uwekezaji zaidi katika wilaya hiyo.”Serikali inaendelea na jitihada za kuvutia viwanda wilaya ya meatu na mkoa wa Simiyu kwa ujumla.
“Kwa sasa Meatu inaviwanda vikubwa vitatu,vidogo 148 na vidogo sana 268 vilivyotoa jumla ya ajira 1342,hivyo nawahakikishia wawekezaji Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwaajili ya kukuza viwanda vya ndani,”alisisitiza.
Rais Samia alisema Kiwanda hicho cha kuchakata pamba cha Biosustain Tanzania Limited kitapanua ajira na uzalishaji wa pamba kwa kiasi kikubwa huku soko likiwepo.
Alisema uwekezaji katika kiwanda hicho ambacho kimezalisha ajira za kudumu 375 na ajira za muda 880 jambo ambalo sio dogo.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema mwaka huu wa 2025 Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha mbolea, viuatilifu na mbegu za pamba zitolewe bure kwa wakulima wa zao la pamba.
“Mwaka huu Mheshimiwa Rais umenipa idhini ya kuwaletea wakulima wa pamba mbolea maalumu ambayo tutaanza kuigawa mwezi wa 10 kwa ajili ya kutumika kwenye zao la pamba, na mbolea hii itagawiwa bure kwa wakulima wa pamba,” alisema Waziri Bashe
Alisema kuwa pamoja na kupata mbegu hizo bure, wakulima hao pia watapata viuatilifu bure na mbegu bure.
“Kwa hiyo mkulima wa pamba mwaka huu atapata mbegu bure, atapata kiuatilifu bure, atapata huduma ya trekta kwa bei ya ruzuku na mbolea bure kwa zao la pamba,” alisema Waziri Bashe
Wakati huo huo Rais Samia ametoa pole kwa wakazi wa Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, kufuatia vifo vya vijana wanne waliofariki dunia katika ajali ya barabarani walipokuwa njiani wakielekea kwenye mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Stendi ya Mabasi ya Meatu jana ambapo yeye alikuwa akihutubia.
Mbali na vijana hao wanne kufariki dunia, watu wengine waliojeruhiwa katika ajali hiyo wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu.
“Kabla sijaendelea ndugu zangu nitoe pole nyingi sana, tumepoteza vijana wetu wanne lakini na wengine kadhaa wameumia katika usafiri kuja kwenye mkutano huu. Nitoe pole sana kwa wana Meatu,” amesema Rais Samia
Mbali na kutoa salamu za pole, Rais Samia Suluhu Hassan amefika katika Hospitali ya Wilaya Meatu ili kuwajua hali majeruhi wa ajali hiyo wanaoendelea kupatiwa matibabu hospitalini.