NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WAFANYAKAZI wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura wa serikali za mitaa ili waweze kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27,mwaka huu.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dk.Angela Muhozya wakati akiongeza na wafanyakazi hao katika kikao cha kupokea ripoti ya tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango mkakati wa taasisi hiyo.
Dk.Angela alisema ni muhimu kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo wakazitumia tarehe 11-20 za mwezi huu kwaajili ya kujiandikisha katika daftari hilo ili ifikapo Novemba 27 wawe na sifa za kupiga kura na kuwachagua viongozi wa serikali za mitaa.
“Tunaelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa ambao umebeba maendeleo ya nchi yetu na yetu binafsi kwa siku za mbeleni, ninawaomba kila mtu katika eneo analoishi aende kujiandikisha ili wakati wa uchaguzi ukifika mkachague viongozi wazuri watakaoshirikiana na wananchi kutuletea maendeleo ya taifa letu”, alisisitiza
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa mpango mkakati huo Dk.Muhozya ambaye ni Daktari Bingwa wa usingizi na wagonjwa mahututi aliwapongeza wafanyakazi hao kwa kujitoa kwao kufanya kazi kwa bidii na kujituma na kuwataka kuongeza jitihada zaidi katika kutoa huduma kwa wananchi.
“Mpango mkakati wetu unaisha mwaka 2025/26 huku ukiwa na maadili ya msingi ya ushirikiano, uadilifu, weledi na ubunifu ninaamini kila mmoja wetu akiyatekeleza haya tutatimiza malengo yetu ya kutoa huduma za moyo zenye uthibitisho, mafunzo na utafiti”, alisema
Akiwasilisha ripoti ya tathimini ya mwaka wa pili wa utekelezaji wa mpango mkakati wa taasisi hiyo Afisa Mipango wa JKCI Vida Mushi alisema walipima kwa kuangalia malengo waliyojiwekea yamefanikiwa kwa kiasi gani, uelewa wa wafanyakazi katika mpango mkakati huo na changamoto zilizopo katika utekelezaji.
“Baada ya kuangalia vipimo tulivyojiwekea tuligundua mpango mkakati wetu kwa mwaka 2024 umefanikiwa kwa asilimia 80 ukilinganisha na mwaka jana ulifanikiwa kwa asilimia 73, ninaamini tukifanya jitihada zaidi tutafikia asilimia 100 katika utekelezaji”.
“Ninawaomba wafanyakazi wenzangu tufanye kazi zetu kwa kufuata malengo ya taasisi ili kuiwezesha taasisi yetu kufika dira yake ya kuwa taasisi inayotambulika kimataifa katika kutoa huduma, mafunzo na kufanya utafiti wa magonjwa ya moyo”, alisema Vida.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Ghati Chacha aliwakumbusha wafanyakazi hao kujaza taarifa zao za kazi wanazozifanya kila siku katika mfumo wa kupima utendaji kazi za watumisi wa umma (PEPMIS) kwa wakati kuliko kusubiri wakati mwaka wa fedha unaisha.
“Majukumu yenu ya kazi mnazozifanya kila siku yako katika mpango mkakati wa taasisi ni muhimu kila wiki mkajaza kazi mlizozifanya kwa wiki husika kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupata alama nzuri za utendaji wa kazi na kuepukana na mzigo wa kujaza kazi za mwaka mzima mwishoni wa mwaka wa fedha”, alisema Chacha