NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Bima la Taifa NIC Insurance kwa mara nyingine limeibuka kuwa mshindi wa kwanza kwenye Sekta ya Bima katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 48 mwaka 2024.
Ushindi wa NIC Insurance ni mwendelezo wa ushindi katika maonesho hayo kwa miaka mitatu mfululizo ambapo imeendelea kuwa kinara.
Akizungumza jijini Dar es salaam Julai 13,2024 katika banda la NIC mara baada ya kukabidhiwa tuzo ya mshindi wa kwanza na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi,ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga Maonesho hayo na kukabidhi vyeti kwa Washiriki,Mkurugenzi Mkuu wa NIC Insurance Kaimu Mkeyenge amesema ushindi huo unatokana na maandalizi mazuri yaliyofanywa na timu nzima ya NIC hivyo anawashukuru kwa kujitoa kwao.
Mkeyenge pamoja na mambo mengine ameonesha kuthamini jitihada zilzofanywa na timu ya Masoko kuhakikisha NIC Insurance inaendelea kutoa huduma nzuri na kutafuta masoko ya Bima kwenye Maonesho hayo hivyo anaamini Bima zitauzika kwa wingi na mwitikio utakuwa mkubwa zaidi.
“Sisi NIC Insurance kama Taasisi ya Umma tumeonekana,Kauli Mbiu ya ‘Sisi ndiyo Bima’imeendelea kujidhihirisha na tumetumia Maonesho haya kama mbinu ya kuuza Bima hivyo tuongeze bidii katika kuuza bima,tutakuja kupimwa kwa namba tu na uwajibikaji hakuna kingine…” amesisitiza na kuhitimisha Mkeyenge