NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Bima la Taifa (NIC) imekuja na Bima ya Maisha ya Majaliwa inayotoa dhamana ya kifedha kwa mteja au wategemezi wa mteja endapo mteja huyo atakuwa amekubwa na janga la kifo.
Akizungumza katika Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Ofisa Bima kutoka NIC, Deogratius Mlumba amesema bima hiyo ni ya miaka mitano hadi 30 na kwamba inampatia fursa mteja kujiwekea akiba kidogokidogo kila mwezi na baadae anapata akiba yake pamoja na faida inayopatikana.
Amesema endapo mteja atakumbwa na janga la kifo wategemezi wake watapatafaida na michango ambayo ilikuwa ikiwekwa na mteja hiyo katika bima hiyo ya maisha.
Mlumba amesema bima hiyo inamfaa mtu yeyote yule anayejiingizia kipata, mfanyabiashara au mfanyakazi kwani kima chake cha chini kabisa cha kuchangia ni kiasi cha Sh. 5000 huku cha juu ni kiasi chochote kile alichonacho mteja.
“Faida ya bima hii inatoa mafao ya Bima ya Maisha yanayozingatia thamani ya mfumko wa bei kwa kulipa zaidi kiasi alichochangia mteja, endapo mteja atapatwa na kifo familia yake itapata fidia ya asilimia 100 ya thamani ya bima,” amesema Mlumba
Aidha amesema Bima hiyo ya Maisha ya Majaliwa ina mafao moja ni mafao ya ukomo pili mafao ya kifo endapo mteja atapatwa muda wowote ndani ya mkataba.
Amesema katika mafao ya kifo ni fidia inayolipwa kwa wategemezi endapo mteja atafariki muda wowote baada ya kujiunga na bima ya Maajaliwa.
Mlumba amesema mafao ya kumaliza mkataba ni mafao ambayo yatalipwa kwa mteja endapo atamaliza muda wake wa mkataba wa Bima ya Maisha ya Majaliwa.
Amesema mteja akishindwa kuendelea kuchangia Bima anaweza kufanya yafaatayo moja ni kupunguza thamani ya Bima ili aweze kuendelea kuchangia au anaweza akaacha kuchangia na kusubiri hadi ukomo wa mkataba wake.