NA MWANDISHI WETU, DODOMA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Chama cha Waagizaji na
Wasambazaji wa Mafuta nchini (TAOMAC) ambapo amewataka wafanyabiashara
hao pamoja na faida wanayoipata wazingatie maslahi wananchi wa hali ya
chini.
Ameyasema hayo Februari 6, 2024 jijini Dodoma katika kikao
ambacho kilijadili masuala mbalimbali ikiwemo changamoto mbalimbali
ambazo wanafanyabiashara hao wanazikabili.
Amesema Serikali siku zote iko tayari kutoa ushirikiano kwa
wafanyabiashara na kuwekea mazingira wezeshi ya biashara zao ili
waweze kuwajibika kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu za usimamizi
katika sekta husika.
“Tunapofanya biashara hii ya mafuta lazima tuangalie mtanzania maskini
ambaye anategemea sekta hii kujikwamua kimaisha, isifike mahala kila
mwisho wa mwezi watu wote wanashika vichwa wakihofia kupanda kwa bei
ya mafuta… Serikali inafanya kila jitihada kupunguza makali ya bei ya
mafuta hivyo nanyi mlizingatie suala hili.”amesema Dk. Biteko
Dk.Biteko ameishukuru TAOMAC kwa ushirikiano wao kwa Serikali katika
kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mafuta ya kutosha na kueleza kuwa
Serikali inatambua na kuthamini mchango wao katika ukuaji wa Uchumi wa
nchi.
Amesema uhusiano uliopo kati ya Serikali na TAOMAC unahitaji kuwa
endelevu na pale zinapotokea changamoto zitafutwe njia za kukabiliana
nazo kwa mstakabali wa Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAOMAC, Kalpesh Mehta ameishukuru
Serikali kwa mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wa mafuta na
utayari wa Serikali kushughulikia changamoto kadhaa zinazojitokeza
katika sekta hiyo.
Akizungumzia mazingira hayo, Mkurugenzi Mtendaji, Raphael Mgaya
amesema ushirikiano wa TAOMAC kwa serikali hauepukiki ili kuhakikisha
nchi inapata mafuta ya kutosha hivyo wapo tayari kushirikiana na
Serikali.
Kikao hicho pia kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Taasisi mbalimbali
za Serikali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Wakala wa Uagizaji wa
Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na
Maji (EWURA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Shirika la
Uwakala wa Meli (TASAC), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiongozwa
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.