- TUANZISHE biashara,
Hilo sasa jambo bora,
Shughuli za mshahara,
Ni zetu si za watoto. - Tuianzishe miradi,
Mingi isiyo idadi,
Kupata kazi ahadi,
Ni zetu si za watoto. - Maisha yanavyokwenda,
Teknoloji yashinda,
Ajira tunazowinda,
Ni zetu si za watoto. - Baadaye yaelekea,
Kazi zaweza potea,
Kazi nazielezea,
Ni zetu si za watoto. - Twawapeleka shuleni,
Huko wako masomoni,
Ajira za duniani,
Ni zetu si za watoto. - Ukizipiga hesabu,
Taratibu taratibu,
Elimu ghali ajabu,
Ni zetu si za watoto. - Watoto waelimika,
Kwa vyeti wanatukuka,
Kazi zao tumeshika,
Ni zetu si za watoto. - Huu muongo wa tatu,
Ajira ndo ziko butu,
Hawazipati wanetu,
Ni zetu si za watoto. - Tuwaandae watoto,
Walijue hili joto,
Kazi zisiwe mvuto,
Ni zetu si za watoto. - Kama tuna biashara,
Watoto wauze sura,
Kazi tubaki vinara,
Ni zetu si za watoto. - Wazijue biashara,
Faida pia hasara,
Kazi za kuweka sera,
Ni zetu si za watoto. - Kama tunao ufundi,
Watoto wawe mafundi,
Ofisi ni za vikundi,
Ni zetu si za watoto. - Na ujasiriamali,
Wajue kusaka mali,
Wasiwe na zetu hali,
Ni zetu si za watoto. - Elimu ni nzuri sana,
Kuidunisha hapana,
Tatizo kazi hakuna,
Ni zetu si za watoto. - Kazi zao watu kumi,
Wakiwemo na wasomi,
Tehama nao uchumi,
Ni zetu si za watoto. - Abaki mtu mmoja,
Tisa waenda kimoja,
Hizo kazi moja moja,
Ni zetu si za watoto. - Kuvijua vitu vingi,
Ni utajiri si bangi,
Njia zetu za vigingi,
Ni zetu si za watoto. - Watoto wetu amka,
Msisinzie amka,
Kazi zinazozeeka,
Ni zetu si za watoto. - Tehama isiwapite,
Bora mbele iwakute,
Wajibu kazi mpate,
Ni zetu si za watoto. - Bahati kazi kuitwa,
Au nyumbani kufwatwa,
Kazi za kufwatwa fwatwa,
Ni zetu si za watoto. - Tulitafutwa zamani,
Ilituende kazini,
Taratibu za zamani,
Ni zetu si za watoto. - Sasa kuna mashindano,
Kupata kazi mavuno,
Shida kazi kubwa mno,
Ni zetu si za watoto. - Muda wa kujiuliza,
Kusomesha tunaweza,
Presha wakimaliza,
Ni zetu si za watoto. - Pengine kujisahau,
Kufikiria walau,
Kupata kazi za dau,
Ni zetu si za watoto. - Elimu kwao mtaji,
Ufundi pia mtaji,
Kazi wapate mtaji,
Ni zetu si za watoto. - Kuwaandaa vizuri,
Waje waile sukari,
Juhudi hizo ni nzuri,
Ni zetu si za watoto. Na Lwaga Mwambande
lwagha@gmail.com 0767223602
KAZI ZINAWEZA KUPOTEA
Leave a comment