- JINSI wasivyokujua, hawatakufuatilia,
Jinsi wanavyokujua, kwao umeshaingia,
Yao yatakusumbua, huna kwa kujifichia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Usiposema ya kwako, utakaa watulia,
Utayajali ya kwako, watu hutafuatilia,
Takuwa kama kituko, nani akuangalia?
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Kimyakimya ukijenga, huna wa kumvutia,
Yako utaungaunga, bila kukushambulia,
Hadhi kubwa utatinga, huku wajisikizia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Ukitaka fanya chako, mwenyewe wajifanyia,
Hunaye pembeni yako, kitu kukuamulia,
Kizuri chako ni chako, mwenyewe chakuvutia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Ukizungukwa na watu, wanaokuangalia,
Ukitaka fanya kitu, ni wengi watakujia,
Kichwani wajaze vitu, usiweze kutulia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Fanya kwa uhuru wako, amani utavutia,
Kwa hayo maisha yako, vita havitakujia,
Taishi kwa raha zako, maisha kifurahia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Kila mtu ni rafiki, tatizo wajipatia,
Watu hawaaminiki, inatufunza dunia,
Jumba bovu wamiliki, laweza kukuangukia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Habari zako za ndani, bora kujimilikia,
Ukimsaka mwandani, zote ukammwagia,
Utazikuta sokoni, ubakie wajutia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Tena wakati mwingine, ni rahisi nakwambia,
Yako yawe kivingine, bila mtu kusikia,
Njia yako uione, peke ukijipitia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Malengo lojipangia, ni rahisi kufikia,
Kama ukikomalia, mwenyewe kizingatia,
Mtu aje kusikia, umeshajimalizia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Usiri wakufundisha, uhuru kushikilia,
Mwenyewe wajifikisha, utakaowafikia,
Wale moyo wakukosha, siyo wa kukuwangia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Kama wote waondoka, mwenyewe unabakia,
Hiyo ni shule hakika, peke yako kubakia,
Hutakuwa na mashaka, jinsi utajiishia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. - Wandugu hawakujali, vile wakuangalia,
Ila sana wanajali, yale unajifanyia,
Mwenyewe ujikubali, ufanye kwa kutulia,
Unapoishi kivyako, kwako uhuru zaidi. Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 076722362
HAWATAKUFUATILIA

Leave a comment