NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
TANZANIA ina fursa ya kuingiza kati ya dola za Marekani bilioni saba hadi 11 kwa mwaka kupitia uongezaji thamani wa aina 11 za madini yakiwemo Madini muhimu na mkakati hatua inayotarajiwa kuongeza mapato ya taifa, kukuza viwanda na kupanua wigo wa ajira.
Akizungumza katika mjadala wa uwekezaji na uongezaji thamani wa madini katika Mkutano wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026) uliofanyika Novemba 19 -21, 2026 jijini Dar Es Salaam, Mkurugenzi wa Manufacturing Africa kutoka McKinsey & Company, Ms Fiker Tadesse Bakele, alisema Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na rasilimali zake za madini iwapo itawekeza katika uzalishaji wa kutosha, uchakataji na upatikanaji wa masoko ya uhakika.
Alisema madini ya kinywe ni miongoni mwa rasilimali zenye fursa kubwa kutokana na uwepo wake nchini na uwezo wake wa kushindana katika soko la kimataifa.
Aliongeza kuwa baadhi ya sampuli za madini hayo zina kiwango cha ubora kinachofikia asilimia 95 ya Total Graphitic Carbon (TGC), jambo linaloweza kuongeza ushindani wake na kuvutia wanunuzi wa kimataifa.
Pia, Bakele alisema Tanzania inapaswa kutumia fursa zilizopo katika madini ya viwandani kama chokaa, calcium na silika, ambayo hutumika kutengeneza saruji, vioo na bidhaa nyinginezo, huku baadhi ya bidhaa hizo zikiendelea kuagizwa kutoka nje ya nchi.
Alisema mkakati huo unaweza kusaidia kukidhi mahitaji ya soko la ndani na baadaye kupanua uzalishaji kwa ajili ya masoko ya kikanda.
Ili kufikia malengo hayo, alieleza Tanzania inapaswa kuhakikisha upatikanaji wa malighafi kwa kiwango kikubwa, soko la uhakika la bidhaa zitakazozalishwa, miundombinu wezeshi, uthabiti wa sera na sheria pamoja na upatikanaji wa mitaji ya kugharamia miradi ya uchakataji.
Akizungumzia ushirikiano wa kikanda, Bakele alisema si lazima kila nchi ijenge kiwanda cha kuchakata kila aina ya madini, bali nchi za Afrika zinapaswa kushirikiana kuwekeza katika viwanda hivyo kwa kuzingatia rasilimali zilizopo katika maeneo mbalimbali.
Alitolea mfano wa Tanzania kuwa na madini ya kinywe na nikeli, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuwa na rasilimali za shaba, huku Burundi pia ikiwa na rasilimali za nikeli.
Alisema ushirikiano huo utasaidia nchi husika kugawana gharama za uwekezaji na kupanua fursa za kuongeza thamani ya madini katika ukanda huo.
Mshirika Mkuu wa Kampuni ya Bowmans Tanzania, Michael Strain, alisema taasisi za Serikali zina nafasi muhimu katika kuwezesha upatikanaji wa fedha za miradi ya madini kwa kushiriki katika tafiti za upembuzi yakinifu na tafiti za kina za kijiolojia.
Alisema tafiti hizo zitasaidia kupata taarifa sahihi kuhusu rasilimali zilizopo, kupanga mifumo bora ya ufadhili na kuhakikisha hatari za uwekezaji zinagawanywa ipasavyo kati ya washirika wa miradi.
Alieleza kwamba taasisi za Serikali zinapaswa kuimarishwa ili ziwe na uwezo wa kuweka sera na mifumo itakayovutia uwekezaji, kusimamia miradi na kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
Amesema ni wajibu wa taasisi hizo kuweka mifumo imara ya usimamizi wa rasilimali ili mapato yatokanayo na madini yatumike katika kujenga maendeleo ya muda mrefu, ikiwemo miundombinu itakayowanufaisha vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Isaac Otolo kutoka Kenya alisema Serikali zinaweza kuongeza uwezekano wa miradi ya madini kutekelezeka kwa kutoa vivutio vya kifedha na kikodi, pamoja na kushiriki moja kwa moja katika umiliki wa hisa na utoaji wa mitaji kwenye miradi hiyo.
Alisema ushiriki wa Serikali katika uwekezaji unaweza kuongeza imani kwa wawekezaji binafsi, hususan wa kigeni, na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali na sekta binafsi.
Alieleza kuwa wawekezaji wanahitaji uhakika wa umiliki wa uwekezaji na ulinzi wa kisheria ili waweze kuwekeza kwa muda mrefu bila hofu ya mabadiliko yanayoweza kuhatarisha mitaji yao.
Alisema mikataba ya ulinzi wa uwekezaji ni miongoni mwa nyenzo muhimu zinazoweza kuhakikisha usalama wa mitaji na kujenga mazingira ya kuaminiana kati ya Serikali na wawekezaji.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda (IDC), Cornwell Mulega, alisisitiza umuhimu wa kuweka mifumo itakayowezesha Serikali na taasisi zake kushiriki kikamilifu katika uwekezaji wa kimkakati ili kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa manufaa ya wananchi.
Aliongeza, ushiriki wa taasisi za Serikali katika miradi ya uwekezaji ni muhimu katika kuhakikisha nchi inanufaika na mapato yatokanayo na rasilimali zake, huku ikiimarisha uwezo wa ndani wa kugharamia na kuendeleza miradi ya uzalishaji na uongezaji thamani wa madini.
Alieleza kuwa kujenga uwezo wa taasisi za ndani, kuimarisha utaalamu na kuweka mifumo ya ushiriki wa mitaji kutasaidia kuongeza manufaa ya sekta ya madini katika uchumi wa taifa.
Walieleza hayo katika mjadala wa uwekezaji na uongezaji thamani wa madini unaoendelea katika Mkutano wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIC 2026), uliolenga kujadili fursa, changamoto na mikakati ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania.






