NA MWANDISHI WETU,DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nishati Dk. Juma Homera amesema zoezi la
uchimbaji wa visima vitatu vya gesi asilia katika Kitalu cha Mnazi Bay
mkoani Mtwara limekamilika kwa mafanikio makubwa, ambapo imegunduliwa
gesi asilia inayotarajiwa kuongeza kiasi cha nishati hiyo kutoka futi
za ujazo trilioni 57.54 zilizopo sasa.
Amesema Serikali inatarajia kuzindua visima hivyo wiki ijayo katika
Kijiji cha Msimbati mkoani Mtwara, ambapo pia itatangaza kiasi cha
gesi asilia kilichogunduliwa kutokana na shughuli hizo za uchimbaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Oktoba 18, 2026, katika Ofisi
Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Homera amesema
visima hivyo, viwili vya uendelezaji na kimoja cha utafiti,
vimechimbwa kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
kwa kushirikiana na mwekezaji, kampuni ya M&P.
Amesema ugunduzi huo unazidi kuiwezesha Serikali kuwa na nishati ya
gesi asilia kwa ajili ya kukidhi mahitaji mbalimbali ya nchi pamoja na
kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta hiyo.
Homera ameongeza kuwa Serikali kupitia TPDC inaendelea na
shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo
mbalimbali nchini, yakiwemo Eyasi-Wembere, Lindi-Mtwara, Songo Songo
Magharibi, Mnazi Bay Kaskazini na Ntorya.
Ameeleza kuwa shughuli za uchukuaji wa data za mitetemo zinaendelea
katika vitalu vya Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara na zinatarajiwa
kukamilika Desemba 2026, huku maandalizi ya uchorongaji wa kisima cha
uzalishaji na usimikaji wa mitambo ya kusafisha gesi yakiendelea
katika Kitalu cha Ntorya.
Kuhusu maendeleo ya Kitalu cha Ntorya, Homera amesema ujenzi wa
bomba la kusafirisha gesi lenye urefu wa kilomita 35 kutoka Ntorya
hadi Madimba umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Desemba
2026, huku uzalishaji wa gesi ukitarajiwa kuanza mapema mwaka 2027 na
kufikia futi za ujazo milioni 40 kwa siku.
Ameeleza kuwa TPDC inaendelea kushirikiana na kampuni binafsi katika
usambazaji wa gesi asilia majumbani na kwenye magari (CNG), ambapo
hadi Septemba 2026, jumla ya vituo 22 vilikuwa vimekamilika na kuanza
kutoa huduma.
Katika hatua nyingine, Homera amesema wiki ijayo Serikali inatarajia
kusaini na kukabidhi leseni mpya za utafutaji mafuta na gesi asilia
(PSA) kwa TPDC, hatua itakayoliwezesha shirika hilo kuendelea na
shughuli za utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa rasilimali hizo
nchini ambapo Makamu wa Rais,Deogratius Ndejembi atakuwa mgeni
rasmi.
Akizungumzia sekta ya umeme, Mhe. Homera amesema uwezo wa uzalishaji
wa umeme nchini umeongezeka na kufikia Megawati 4,646 kutoka vyanzo
mbalimbali, ikiwemo maji, gesi asilia, jua na nishati nyingine
mbadala, huku Serikali ikiendelea kutekeleza mkakati wa kuongeza uwezo
huo hadi Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Amesema katika kuimarisha uzalishaji wa umeme kwa kutumia nishati
jadidifu, Serikali imekamilisha Mradi wa Kishapu I wenye uwezo wa
kuzalisha Megawati 50 za umeme wa jua, huku ujenzi wa Kishapu II wenye
uwezo wa Megawati 100 ukiendelea.
Aidha, miradi mingine yenye uwezo wa zaidi ya Megawati 600 ipo katika
hatua mbalimbali za majadiliano na upembuzi.
Kuhusu miundombinu ya usafirishaji umeme, Waziri huyo amesema Serikali
imekamilisha Mradi wa Chalinze–Dodoma tangu Septemba 2026, ambao
umeimarisha ubora na kiwango cha umeme kinachofika katika mikoa ya
Magharibi na Kaskazini mwa nchi.
Ameongeza kuwa Mradi wa Iringa–Tunduma–Sumbawanga unatarajiwa kuwashwa
Novemba 2026 na kuunganisha Mkoa wa Rukwa katika Gridi ya Taifa kwa
mara ya kwanza, huku Mradi wa Chalinze–Kinyerezi–Mkuranga ukitarajiwa
kuwashwa Februari 2027 ili kuimarisha upatikanaji wa umeme jijini Dar
es Salaam na maeneo ya viwanda ya Mkuranga.
Aidha, amesema utekelezaji wa Mradi wa Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika
unaendelea kwa kasi, ukiwa na lengo la kuunganisha mikoa ya Lindi na
Mtwara katika Gridi ya Taifa na kuondoa changamoto za upatikanaji wa
umeme katika maeneo hayo.

