NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Nishati,Dk. Juma Homera, amezindua mifumo
mipya ya kuhudumia wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
pamoja na Mkataba wa Huduma kwa Wateja ulioboreshwa, ikiwa ni hatua
inayolenga kuhakikisha wateja wakubwa na wadogo wa Shirika hilo
wanapata huduma kwa haraka na urahisi.
Akizindua mifumo hiyo jijini Dar es Salaam leo Jumanne Oktoba 6, 2026, Dk
Homera amesema TANESCO imeonesha dhamira ya kupiga hatua zaidi katika
kuboresha huduma kwa wateja, akieleza kuwa hatua hiyo ina umuhimu
mkubwa katika maslahi ya Taifa, hususan katika utekelezaji wa Dira
2050 na maono ya Rais, Dk.Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha
taasisi zinatumia ubunifu na teknolojia katika kuboresha huduma kwa
wananchi.
Mifumo aliyoizindua ni pamoja na ‘Twiga Assistant’ suluhisho la kisasa
linalotumia akili mnemba (AI) na kumwezesha mteja kupata huduma saa 24
kwa siku bila kulazimika kupiga simu TANESCO na ‘Twiga Premium
Portal’ jukwaa maalum la kidijitali litakalowawezesha wateja wakubwa
kupata huduma mbalimbali kwa urahisi zaidi.
Aidha, Dk. Homera amezindua namba maalum 185 kwa ajili ya wateja
wakubwa, itakayowawezesha kupata huduma za haraka, za moja kwa moja na
zenye kipaumbele pamoja na uzinduzi wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja
Wakubwa ili kuhakikisha kundi hilo linapata huduma zinazokidhi
mahitaji yake.
Pamoja na kuipongeza TANESCO kwa ubunifu huo uliofanywa na wataalamu
wa ndani, Dk. Homera amelitaka Shirika hilo kuhakikisha Mkataba wa
Huduma kwa Wateja unatekelezwa kwa vitendo katika ngazi zote na ahadi
zilizomo ndani yake zinakuwa sehemu ya utamaduni wa kazi wa kila
mtumishi. Pia, amesisitiza mifumo yote iliyozinduliwa ifanye kazi kwa
ufanisi muda wote na itumike kwa vitendo ili kuleta matokeo
yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Vilevile, ameelekeza TANESCO kutoa elimu ya kutosha kwa makundi yote
ya wateja kuhusu mifumo hiyo na namna ya kuitumia kupata huduma na
kutatua changamoto mbalimbali.
Ameitaka pia TANESCO kuongeza matumizi ya takwimu na maoni ya wateja
katika kufanya maamuzi, huku kila lalamiko la mteja likitumika kama
fursa ya kuboresha huduma.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda taarifa za wateja na mifumo ya
kidijitali kwa kuzingatia sheria na viwango vya usalama wa taarifa,
sambamba na kukiwezesha kikamilifu Kitengo cha Huduma kwa Wateja
Wakubwa kutoa huduma bora na kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Dk.Homera amesema uwekezaji unaofanywa na
Serikali katika Sekta ya Nishati umeendelea kuimarisha upatikanaji wa
umeme wa uhakika nchini, ambapo uwezo wa kuzalisha umeme umefikia MW
4,606, sawa na ongezeko la asilimia 21.32, huku mahitaji ya juu ya
umeme yakifikia MW 2,316, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12.97
ikilinganishwa na mwaka 2025.
Amesema ongezeko hilo la mahitaji ya umeme linaenda sambamba na
kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaohitaji kuhudumiwa, hivyo mifumo
hiyo mipya itachangia utekelezaji wa malengo ya Serikali, ikiwemo Dira
ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotambua nishati kuwa kichocheo muhimu
cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya nchi.
Katika hafla hiyo, Dk.Homera amesisitiza utekelezaji wa maelekezo ya
Rais, Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Tanzania inafikia
uwezo wa kuzalisha megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030 akieleza kuwa
lengo hilo linawezekana kutokana na Wizara na taasisi zake, ikiwemo
TANESCO, kuwa na wataalamu wanaofanya kazi kwa weledi, sambamba na
kuendelea kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, ukiwemo Mradi
wa Umeme wa Jua wa Kishapu ambao awamu yake ya pili inahusisha MW 100
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia
Mafuta na Gesi Asilia, Dk.James Mataragio, amesema huduma
zilizozinduliwa, zikiwemo Twiga AI Chatbot, Twiga Premium Customer
Portal, Premium Customers Toll Free Line, Premium Customer Service
Section pamoja na Mkataba wa Huduma kwa Wateja ulioboreshwa,
zinaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa pamoja na
kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini, huduma zinazotolewa kwa
wananchi zinaendelea kuboreshwa kupitia teknolojia, ubunifu na mifumo
ya kisasa.

