NA BEATUS MAGANJA,MOROGORO
WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dk. Ashatu Kijaji (Mb) ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kwa mafanikio yake katika kuvutia wawekezaji jambo lililotajwa kuchangia ongezeko la mapato ya Taasisi hiyo, huku akiielekeza Menejimenti ya mamlaka hiyo kuandaa mikakati ya muda mfupi, ya kati na ya muda mrefu ya kudhibiti migongano baina ya wanyamapori na binadamu.
Akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya TAWA alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA mkoani Morogoro Julai 7, 2026, Dk. Kijaji alisema mwaka mpya wa fedha unapaswa kuwa mwanzo wa utekelezaji wenye matokeo makubwa katika kuimarisha uhifadhi wa maliasili na kuongeza kasi ya kudhibiti migongano kati ya binadamu na wanyamapori ili kuhakikisha usalama wa wananchi na wanyamapori kwa pamoja.
“Tunapaswa kuwa na mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu itakayowezesha kupunguza migongano kati ya wanyamapori na binadamu. Lengo letu ni kuona wananchi wanakuwa salama na wanyamapori wanaendelea kuhifadhiwa” alisema Dk. Kijaji.
Aidha, Waziri huyo aliielekeza TAWA kuendelea kuimarisha ushirikiano na wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi, akisisitiza kuwa wananchi ndiyo walinzi namba moja wa rasilimali za wanyamapori. Pia alisisitiza kuimarishwa kwa ulinzi wa maeneo ya hifadhi kwa kutoruhusu shughuli za kibinadamu ndani ya maeneo hayo, ikiwemo uvamizi kwa ajili ya kilimo na matumizi mengine yasiyoruhusiwa kisheria.
Vilevile Waziri Kijaji aliipongeza TAWA kwa usimamizi mzuri wa fedha za Serikali hususan katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na matumizi ya teknolojia katika shughuli mbalimbali za uhifadhi.
Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis R. Semfuko, alisema kuimarika kwa ulinzi na usimamizi wa rasilimali za wanyamapori kumechangia ongezeko la idadi ya wanyamapori katika maeneo yanayosimamiwa na mamlaka hiyo.
Alisema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2025, idadi ya swala aina ya Puku imeongezeka kutoka 1,950 mwaka 2021 hadi 3,185 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 63.
Aidha, kaya 1,107 zilizokuwa katika Kijiji cha Ngombo, Wilaya ya Malinyi zimehama kutoka ndani ya Pori la Akiba Kilombero kufuatia utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi.
Semfuko alisema TAWA pia imeendelea kuimarisha uwekezaji baada ya kusaini mikataba mitatu ya uwekezaji mahiri na kufikisha jumla ya maeneo 16 ya uwekezaji huo, ambao kwa sasa unachangia asilimia 46 ya mapato ya mamlaka.
Vilevile, idadi ya watalii wa picha imeongezeka na kufikia 267,575 ikilinganishwa na watalii 240,967 waliotembelea maeneo yanayosimamiwa na TAWA katika mwaka wa fedha 2024/25.
Aliongeza kuwa TAWA imeimarisha mwitikio wa matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kwa kukamilisha ujenzi wa mabwawa 14, vizimba 31 na vituo 14 vya askari, hatua iliyochangia kuokoa maisha ya wananchi na mali zao.
Aidha, gawio la Sh. Bilioni 9.7 limetolewa kwa WMA 16, vijiji 161 na Halmashauri za Wilaya 41, huku maelfu ya wananchi wakiendelea kunufaika na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika maeneo ya hifadhi.
Kwa upande wa utendaji wa taasisi, alisema TAWA pia imeajiri watumishi 661 kuongeza nguvu kazi na kufikia makusanyo ya shilingi bilioni 92.28 hadi Juni 2026, ikilinganishwa na shilingi bilioni 87.32 zilizokusanywa mwaka uliotangulia.
Katika ziara hiyo, Dk. Kijaji aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi, pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara,Bernard Marcelline.
Ziara hiyo imeendelea kudhihirisha dhamira ya Serikali ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori ili kuleta manufaa kwa wananchi, sambamba na kutafuta mwarobaini wa kukabiliana na changamoto za migongano baina ya wanyamapori na binadamu.

