NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WATUB wanaojitolea kutoka Japan (JOCV) chini ya Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Maofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Tanzania na Japan, wamehimiza wanawake kutumia ujuzi walionao kujikwamua kiuchumi kupitia ujasiriamali, hususan kwa kutumia taka kutengeneza bidhaa mbalimbali za mapambo na kazi za mikono.
Wamesema ubunifu unaotokana na mazingira unaweza kuwa chanzo kikubwa cha kipato endapo utaunganishwa na soko na uthubutu wa kuanzisha biashara.
Mpango huo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya huduma za kujitolea za JICA (JOCV) nchini Tanzania.
Katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), wakujitolea kutoka JICA wamewasilisha bidhaa mbalimbali zinazotengenezwa na vikundi vya wanawake zikiwemo sabuni za mikono, mapambo ya nywele yaliyosokotwa kwa uzi na hereni zinazotengenezwa kwa vifuniko vya chupa za plastiki vilivyorejelewa.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Aisha Lugendo, amesema wanawake hao walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali yaliyowawezesha kutumia uzi, sindano na plastiki kutengeneza bidhaa zenye thamani ya kibiashara.
Amesema zaidi ya wanawake 20 walipata mafunzo mwanzoni mwa mradi huo, huku wanawake 10 wakiendelea na uzalishaji wa bidhaa hizo na kujipatia kipato kupitia biashara hiyo.
Kwa mujibu wa Lugendo, bidhaa hizo zimekuwa zikipata soko, ingawa changamoto kubwa inayowakabili bado ni upatikanaji wa masoko ya kudumu.
Naye Masahiko Konishi, Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka Kata ya Kidhesa, Iringa, amesema wakisherekea miaka 60 tangu kuanza kwa program hiyo ya kujitolea wamekuwa wakishirikiana na wanawake katika kuwafundisha uundaji wa bidhaa za mapambo kama vibanio vya nywele na hereni kwa kutumia malighafi za ndani, akibainisha kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa soko la uhakika licha ya bidhaa hizo kupendwa na jamii.
Ameongeza kuwa ushiriki wao katika Maonesho ya Sabasaba mwaka huu unalenga kutangaza bidhaa hizo, kupanua wigo wa masoko na kuongeza kipato kwa wanawake wanaoshiriki katika mradi huo.
Aidha, Akane Miyazaki, Mtaalamu wa Mazingira kutoka Manispaa ya Morogoro, amesema amekuwa akifundisha jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa taka, huku akibainisha kuwa taka za plastiki zinaweza kubadilishwa kuwa bidhaa zenye thamani kama hereni na mapambo mbalimbali, hivyo kuchangia katika uhifadhi wa mazingira na kuongeza kipato kwa wananchi.

