NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Emmanuel Nchimbi amewataka wazalishaji wote nchini kutumia alama ya ‘Made in Tanzania’ ili kujenga imani ya bidhaa zinazozalishwa nchini na kuongeza ushindani wake katika masoko ya kimataifa.
Dk. Nchimbi ameyasema hayo Julai 6, 2026 wakati wa kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Dhahabu ya miaka 50 ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Dk. Nchimbi amesema alama hiyo ya ubora ni muhimu katika kuitangaza Tanzania na kutambulisha bidhaa bora zinazozalishwa nchini.
“Kuanzishwa kwa alama maalumu ya ‘Made in Tanzania’ kutaleta heshima kwa taifa kwa kutambulisha bidhaa bora zinazozalishwa nchini,” amesema Dk. Nchimbi.
Aidha Makamu wa Rais pia amezitaka taasisi zinazosimamia viwango kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi ili kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinakidhi viwango vya kimataifa, hatua itakayosaidia kulinda heshima ya taifa na kupanua masoko ya bidhaa hizo duniani.
Dk. Nchimbi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka sera rafiki, kuimarisha miundombinu na kushirikiana na sekta binafsi ili kujenga uchumi wa viwanda wenye ushindani na kufanikisha azma ya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati.
Amezipongeza taasisi za fedha kwa kuendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa viwanda vidogo, akieleza kuwa hatua hiyo imechangia kupunguza vikwazo vya mitaji kwa wajasiriamali wengi.
Hata hivyo Dk. Nchimbi amesema maono ya Serikali ni kuona Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) yakibadilika kutoka eneo la kuonesha bidhaa pekee na kuwa kitovu cha ubunifu, utafiti, teknolojia na biashara za kimataifa ifikapo mwaka 2050.
Amesema ili kufanikisha maono hayo, ni muhimu kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara na kuhakikisha viwanda vinapata mitaji ya kutosha, akizitaka taasisi za fedha kuongeza mikopo kwa viwanda vidogo na vya kati kwa masharti nafuu yatakayowawezesha wafanyabiashara wengi zaidi kukuza uzalishaji.
Awali akizungumza,Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema mauzo ya bidhaa na huduma za Tanzania nje ya nchi yameongezeka kwa kiwango kikubwa huku mauzo ya nje yakifikia takribani Dola za Marekani Bilioni 18.6 huku mauzo ya bidhaa yakifikia Dola za Marekani bilioni 11 yakionesha ongezeko la asilimia 11.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dk. Latifa Khamis amewataka watanzania kuendelea kulitumia jukwaa la maonesho ya sabasaba kujitangaza katika medani za kimataifa za kibiashara.
Dk. Khamis amewataka pia wafanyabishara kuitangaza Tanzania kimataifa kutokana na ukubwa wa maonesho hayo ya sabasaba yanayohudhuriwa na watu kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Amesema TanTrade itaendelea kutengeneza mazingira wezeshi kwa wafanyabishara nchini kuyafikia masoko ya kimatiafa.

