NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
WANANCHI wa Dar es Salaam na mikoa jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayotarajiwa kuanza rasmi Juni 28 mwaka huu, huku maadhimisho ya mwaka huu yakipewa hadhi ya kipekee kutokana na kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa Juni 12,2026 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda wakati alipofanya ziara ya kukagua maandalizi ya maonesho hayo, ambapo amesema mwaka huu ni wa kihistoria kwa kuwa maonyesho hayo yanaadhimisha nusu karne tangu yalipoasisiwa na kuwa jukwaa muhimu la biashara, uwekezaji na utangazaji wa bidhaa mbalimbali.
“Mwaka huu ni wa kipekee kidogo kwa sababu maonyesho haya yanatimiza miaka 50 tangu yalipoasisiwa. Hivyo nawaomba wananchi wa Dar es Salaam na mikoa jirani wajitokeze kwa wingi kushiriki maadhimisho haya muhimu,” amesema Mapunda
Amesema baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya maonyesho, ameridhishwa na hatua kubwa iliyofikiwa katika maandalizi, ingawa alibainisha kuwa baadhi ya mabanda yaliyopo katika Ukumbi wa Karume, yanayotumiwa na taasisi za serikali, halmashauri na manispaa, bado yanahitaji kuongeza kasi ya ukamilishaji.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka wadau wote wenye mabanda kuhakikisha wanakamilisha maandalizi yao mapema kabla ya tarehe ya ufunguzi ili wageni watakaojitokeza washuhudie mandhari inayostahili hadhi ya maadhimisho ya miaka 50 ya Sabasaba.
“Tunataka kabla ya tarehe 28 mabanda yote yawe yamekamilika na kupambwa vizuri ili wageni wetu wakifika waone kweli kwamba haya ni maonyesho maalumu ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake,” amesisitiza.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alisema maonesho ya mwaka huu yatakuwa na vivutio vingi zaidi, ikiwemo fursa za utalii, bidhaa mbalimbali za ndani na nje ya nchi pamoja na bidhaa adimu ambazo si rahisi kupatikana katika maeneo mengine.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) Dk. Latifa Khamis amesema maonesho ya mwaka huu yatakuwa makubwa na ya kipekee kuliko wakati mwingine wowote kutokana na maadhimisho ya Golden Jubilee, huku waandaaji wakiahidi programu mbalimbali zitakazounganisha biashara, burudani, uwekezaji na fursa za kimataifa.
“Tunasherehekea miaka 50 ya maonesho yetu. Tumejipanga kuhakikisha maonesho haya yanakuwa makubwa na ya aina yake. Programu tulizoandaa zitamfanya mwananchi anapokuja hapa asitamani kuondoka haraka,” amesema
Alieleza kuwa TanTrade imejizatiti kuhakikisha kila mshiriki, kuanzia wafanyabiashara, wawekezaji, watafiti hadi wananchi wa kawaida, wanapata fursa ya kujifunza, kufanya biashara na kujenga mitandao ya kikazi kupitia maonesho hayo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, hadi sasa nchi 23 zimekamilisha uthibitisho wa kushiriki maonesho hayo huku kampuni 256 kutoka nje ya Tanzania yakiwa tayari yamejiandikisha.
Aidha, zaidi ya kampuni 2,776 ya ndani nayo yamehakikisha uwepo wake katika tukio hilo kubwa la biashara kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Hata hivyo amesema mbali na shughuli za biashara, maonesho ya mwaka huu yataambatana na programu mbalimbali za burudani na kijamii zenye lengo la kufanya maadhimisho ya miaka 50 kuwa ya kukumbukwa.
“Miongoni mwa programu hizo ni pamoja na matembezi ya kuadhimisha miaka 50 ya Sabasaba yatakayolenga kuhamasisha matumizi na uendelezaji wa bidhaa zenye nembo ya Made in Tanzania, pamoja na usiku wa Golden Jubilee utakaowakutanisha wadau mbalimbali wa maonesho hayo,” amesema
Aidha, amesema usiku wa Golden Jubilee utakaofanyika Julai 6 utatumika kutoa tuzo kwa washiriki, taasisi na wadau waliotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya maonesho hayo kwa kipindi cha miaka 50.
“Wapo washiriki ambao wamekuwa nasi kwa miongo kadhaa. Wameendelea kushiriki kila mwaka na hata watoto wao wameendeleza ushiriki huo. Hawa ni sehemu ya historia ya Sabasaba na wanastahili kutambuliwa,” amesema.
Maonesho ya Sabasaba ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa zaidi ya jukwaa la biashara, yakijikita pia katika burudani, ubunifu, uwekezaji, utalii na ujenzi wa mitandao ya kibiashara, huku maelfu ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi wakitarajiwa kuhudhuria.

