NA MWANDISHI WETU,MPANDA,KATAVI
KUFUATIA ukaguzi uliofanywa kwa wamiliki wa leseni wanaofanya uchimbaji kwenye mto na kuathiri mazingira, Waziri wa Madini Anthony Mavunde ametoa maelekezo ya kusimamishwa kwa shughuli za uchimbaji madini kwenye mto huo mkoani hapa.
Ametoa kauli Mei 13, 2026 alipofanya ziara ya ukaguzi wa shughuli za uchimbaji madini katika Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Nsimbo.
“Mhe. Rais ametupa maelekezo mahususi Wizara ya Madini kuhakikisha shughuli zote za uchimbaji zinafanyika kwa mujibu wa Sheria na zisilete athari kwenye mazingira. Tumeshuhudia sote kinachofanyika hapa ni kinyume na matakwa ya Sheria yetu ya Madini Sura 123”
“Hivyo, naelekeza kuanzia leo shughuli zote za uchimbaji zisimame hadi pale mtakapotekeleza wajibu wenu kama mlivyoelekezwa na Ofisa Madini Mkazi wa Katavi kupitia barua aliyowaandikia. Pia, wamiliki wa leseni wasilisheni mpango wa kuhifadhi mazingira kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji tena”, alisisitiza Waziri Mavunde.
Vilevile, Waziri Mavunde alifanya ukaguzi wa mikataba ya msaada wa kiufundi (TSA) waliyoingia wachimbaji wadogo wa kitanzania na wawekezaji wa nje na kubaini mapungufu ambayo yalipelekea kuagiza Ofisi za Afisa Madini Wakazi wa Mikoa ya kimadini kufanya ukaguzi wa mikataba ya TSA nchi nzima ili kubaini iwapo inawanufaisha watanzania na inazingatia matakwa yaliyowekwa kisheria.
Akieleza utatuzi wa changamoto ya ukosefu wa maeneo ya uchimbaji, Mavunde alitoa maelekezo kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kutoa Hati ya Makosa (Default Notice) kwa wamiliki wote wa leseni za utafiti wasioendeleza na kufuata masharti ya leseni hizo.
“Lengo ni kuyafuta maeneo yote ya leseni za utafiti yasiyoendelezwa na kuyagawa kwa wachimbaji wadogo kupitia vikundi vyao. Aidha, maeneo mengine yatatumika kugawa maeneo kwa wachimbaji wadogo vijana, wanawake na wenye ulemavu kupitia programu ya Mining for A Brighter Tommorow (MBT)” alibainisha Waziri Mavunde.
Akibainisha juu ya leseni alizozifuta mwezi uliopita, Waziri Mavunde alitangaza kutenga leseni tatu za utafiti ili zigawiwe kwa wachimbaji wadogo mkoani Katavi, ambapo wachimbaji wadogo walishukuru na kupongeza jitihada zinazofanywa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuwasikiliza changamoto zao na kuzitatua kwa wakati.
Awali, Mavunde alieleza kuwa amefika kufanya ziara Mkoani Katavi kufuatia maelekezo ya Dk.Mwigulu Nchemba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa alipofanya ziara ya kikazi mkoani Katavi.
Akitoa maelezo ya Mkoa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu aliishukuru Serikali kwa hatua za utatuzi wa changamoto za wachimbaji Mkoani Katavi na kuahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri wa Madini yanakwenda kusimamiwa ipasavyo ili yalete tija na kuimarisha shughuli za uchimbaji.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Haidary Sumry na Anna Lupembe, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo walimshukuru Rais kwa kuendelea kuisimamia ipasavyo Serikali ambayo imekuwa ni mhimili imara katika kutatua changamoto za wananchi wa Majimbo yao.












