NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Davidi Nchimbi, amesema kuwa Shirika litaendelea kupanua huduma za intaneti ya kasi (Faiba) nchini ili kuchochea maendeleo ya kidijitali na kiuchumi.
Akizungumza katika uzinduzi wa Kituo cha Kijitonyama cha FTTx Experience Center, Nchimbi alisema kituo hicho ni jukwaa muhimu litakalowawezesha wananchi kujionea kwa vitendo namna teknolojia ya kisasa ya mawasiliano inavyoweza kuboresha maisha yao ya kila siku katika nyanja za elimu, biashara na huduma za kifedha.
Alisema TTCL inaendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Biashara wa miaka 10 ulioanza mwaka wa fedha 2025/26, unaolenga kuongeza ufanisi, ubunifu na mapato ya Shirika.
Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, Shirika lilipata faida ya Sh.Bilioni 22.9 kabla ya kodi, hatua inayodhihirisha mwelekeo chanya wa kiutendaji.
Nchimbi pia aliwashukuru wadau wa maendeleo wakiwemo kampuni za Huawei na Hisense kwa kuendelea kushirikiana na TTCL katika kuleta teknolojia za kisasa zinazochochea ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema uzinduzi wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa Shirika wa kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza upatikanaji wa intaneti ya kasi nchini.
Alieleza kuwa kupitia kituo hicho, wateja watapata fursa ya kujifunza na kujionea matumizi ya teknolojia ya Faiba (Fiber To The X – FTTx) katika mazingira ya nyumbani, ofisini na maeneo ya biashara, sambamba na huduma zilizounganishwa (Converged Services) zinazowezesha kupata intaneti, simu na vifurushi vya data katika mfumo mmoja.
Marwa aliongeza kuwa TTCL inaendelea kusambaza huduma ya “Faiba Mlangoni Kwako” katika mikoa mbalimbali nchini, hatua inayolenga kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuhakikisha huduma za mawasiliano zinakuwa bora na za uhakika.
Uzinduzi wa Kituo cha Kijitonyama FTTx Experience Center unatajwa kuwa ni hatua muhimu katika juhudi za TTCL za kujenga Tanzania ya kidijitali, huku ukitoa nafasi kwa wananchi kujifunza, kutumia na kunufaika na teknolojia za kisasa za mawasiliano.





