NA MWANDISHI WETU,IFAKARA,KILOMBERO
INGAWA ni miaka minne imesalia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2030, joto la kisiasa limeanza kupanda kwa kasi katika Jimbo la Kilombero mkoani Morogoro.
Hii ni baada ya kuibuka kwa taarifa zinazomhusisha Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Peter Lijualikali, na harakati za chini kwa chini za kutaka kurejea kwenye kiti hicho alichokishikilia kati ya mwaka 2015 na 2020.
Vyanzo vyetu kutoka kata ya Mwaya vimepenyeza picha na taarifa zikimuonesha Mkuu huyo wa Wilaya akishiriki matukio ya kijamii mnamo Aprili 7, 2026 Kata ya Mwaya,ambapo alishiriki Msiba wa mtoto wa mmoja wa wapambe wake aliyetajwa kwa jina la Kumburu.
Inadaiwa kuwa Lijualikali amekuwa akionekana jimboni humo mara kwa mara huku akigawa pesa kiasi cha Sh.30,000 kama posho jambo linalotajwa na wapinzani wake kama mbinu ya mapema ya “kupiga kampeni” na kusafisha njia kuelekea uchaguzi wa ndani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tuhuma za Vikao vya Usiku na “Kupanga Safu”
Mbali na ushiriki wa misiba, taarifa zinasema DC huyo amekuwa akifanya vikao vya faragha nyakati za usiku na baadhi ya viongozi wa matawi.
Lengo la vikao hivyo linatajwa kuwa ni kuandaa “safu” ya uongozi kuelekea Uchaguzi wa Ndani wa CCM unaotarajiwa kufanyika mwakani 2027 ili kujihakikishia ushawishi wa kutosha wakati wa kura za maoni za ubunge.
CCM Wilaya yatoa neno.
Akizungumza kwa njia ya simu, Katibu wa CCM Wilaya ya Kilombero, Gervas Ndaki, amekiri kupokea taarifa hizo na tayari wameanza uchunguzi ili kubaini ukweli ya jambo hilo.
“Nasi tumesikia taarifa hizo tunazifanyia uchunguzi na pindi tutakapo baini ukweli tutatolea taarifa ” alisema Ndaki.
Katibu huyo aliongeza kuwa si jambo jema kwa mteule wa Rais kuanza kampeni za mapema na ikibainika kama kweli hatua zitachukuliwa dhidi yake.
Lijualikali Ajitetea:
“Kilombero ni Nyumbani”
Kwa upande wake,Lijualikali amekanusha vikali tuhuma za kuanza kampeni.
Akifafanua ushiriki wake katika msiba wa mzazi wa rafiki yake, Lijualikali alisema Kilombero ni nyumbani kwao na ana haki ya kurudi wakati wowote anapokuwa na likizo au matatizo ya kifamilia bila kuharibu utendaji kazi wake wa kila siku.
“Ndugu mwandishi, mimi Kilombero siyo jimboni kama wanavyopaita wengine, mimi Kilombero ni nyumbani kwetu. Ndugu zangu wapo kule, marafiki wapo pale. Sasa hata sitakiwi kurudi nyumbani hata nikifiwa au nikiwa likizo?” alihoji DC huyo.
Aidha, alitolea ufafanuzi kuhusu kiasi cha fedha alichotoa kama rambirambi kwenye msiba wa mtoto wa rafiki yake
Kumburu akisema: “Ni kweli nilitoa rambirambi ya Sh.250,000/- kwa rafiki yangu Kumburu baada ya kufiwa na mtoto wake na siyo 30,000 kama inavyoelezwa na baadhi ya watu na kusema kuwa hajawahi kufanya kikao chochote cha siri na viongozi wa Chama iwe mchana au usiku na kama yupo mwenye picha za vikao hivyo vya usiku awatumie kama alivyotuma za msibani.” alimalizia Lijualikali.
Wadau na Wachambuzi wa siasa mkoani Morogoro wanaona kuwa kurejea kwa Lijualikali kwenye ulingo wa Kilombero, jimbo ambalo aliliwahi kuliongoza kutaibua upinzani mkubwa ndani na nje ya chama kwa kuzingatia ni siku chache tu zimepita tangu wananchi wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kuvutiwa na utendaji wa DC Lijualikali na kumuomba waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Mwigulu Nchemba kumuhamishia DC huyo wa Nkasi kwenye wilaya ambayo kwa sasa anakaimu.

