NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dk. James Mataragio amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayebainika kuficha mafuta kwa lengo la kuyauza baadaye kwa bei ya juu, akisisitiza kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa.
Mataragio ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kutembelea maghala ya kuhifadhia mafuta ya Kampuni ya Camel Oil yaliyopo Kurasini jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kufuatilia hali ya upatikanaji wa mafuta nchini.
Amesema lengo la ziara hiyo ni kujiridhisha kuhusu uwepo wa akiba ya mafuta na mwenendo wa usambazaji wake, kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya vituo vya mafuta vinavyodai kucheleweshewa huduma au kutopata mafuta kwa wakati.
“Tumesikia kelele kwamba kuna baadhi ya vituo havipati mafuta au kuna ucheleweshaji wa makusudi katika upakiaji, ndiyo maana tumekuja kujionea hali halisi. Serikali inataka kuhakikisha mafuta yanapatikana na yanafika katika vituo vyote nchini,” amesema Mataragio.
Ameongeza kuwa Serikali imelenga kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha ya mafuta, huku akibainisha kuwa hakuna uhaba wa mafuta kwa sasa na yanatosheleza mahitaji ya wananchi.
Aidha, Mataragio amesema changamoto mojawapo inayojitokeza ni hofu miongoni mwa wafanyabiashara wadogo, hali inayowasababisha kununua mafuta kwa wingi kupita mahitaji yao, jambo linaloweza kuchangia kuonekana kwa uhaba usio wa kweli.
“Sisi Serikali tunawahakikishia Watanzania kwamba mafuta yapo ya kutosha, hivyo hakuna sababu ya kununua mafuta kwa wingi au kuficha. Hali hiyo inaweza kusababisha uhaba bandia,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, amewapongeza Kampuni ya Camel Oil kwa kuendelea kutoa huduma usiku na mchana, akiwataka kudumisha hali hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho baadhi ya wafanyabiashara wanajaribu kutumia fursa ya soko kujinufaisha kwa njia zisizo halali.
Mataragio pia amegusia athari za vita inayoendelea Mashariki ya Kati, akisema imeathiri soko la mafuta duniani, lakini amesema kuwa Tanzania imejipanga vyema na ina akiba ya kutosha inayoweza kuhudumia nchi hadi mwezi Julai mwaka huu.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Dk. James Andilile, amesema changamoto za upatikanaji wa mafuta duniani zimetokana na athari za vita hiyo, akibainisha kuwa Tanzania inaagiza sehemu kubwa ya mafuta kutoka Mashariki ya Kati.
Amesema Serikali ilichukua hatua mapema kuhakikisha upatikanaji wa mafuta unaendelea kuwa salama, huku akisisitiza kuwa hakuna uhaba wa mafuta nchini kwa sasa.
Hata hivyo, ameeleza kuwa kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na uagizaji mafuta kutokana na uharibifu wa miundombinu katika maeneo ya vita kumeongeza gharama za mafuta katika soko la dunia, hali inayoweza kuathiri upangaji wa bei nchini.
“Tunaagiza mafuta kwa kutumia dola, hivyo ongezeko la gharama katika soko la dunia lina maana kwamba tunaweza kuagiza mafuta yale yale kwa gharama kubwa zaidi,” amesema Dk. Andilile.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Camel Oil, Salrh Bajber amesema kampuni hiyo inaendelea kutoa huduma kama kawaida na ina akiba ya kutosha ya mafuta.
Ameeleza kuwa kwa mwezi Aprili wameagiza lita milioni 70 za mafuta kwa ajili ya maghala yao, huku kwa mwezi Mei wakitarajia kuingiza lita milioni 84 kwa ajili ya usambazaji.
Aidha, amesema hadi Machi 25, 2026, kampuni hiyo imesambaza zaidi ya lita milioni 44 za mafuta, huku ikiwa na oda zinazoendelea za takribani lita milioni tano ambazo ziko katika hatua za upakiaji.
Kwa ujumla, Serikali imewataka wafanyabiashara na wananchi kuondoa hofu, ikisisitiza kuwa mafuta yapo ya kutosha na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kuvuruga utaratibu wa soko.




