NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
KAMPUNI ya GF Trucks and Equipment imeeleza kufurahishwa na mafanikio yake katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ikijivunia kupata tuzo ya banda bora kwa mwaka wa pili mfululizo huku ikiahidi kuendelea kuleta teknolojia bunifu na rafiki kwa mazingira.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, mwakilishi wa kampuni hiyo, Salman Karmali, alisema kampuni hiyo imekuwa mshiriki mzuri wa maonesho hayo tangu kuanzishwa kwake na imeendelea kutumia jukwaa hilo kuwatambulisha Watanzania bidhaa na teknolojia mpya.
Alisema maonesho ya mwaka huu, yanayoadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, yamevutia idadi kubwa ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi, jambo lililochochewa na kampeni kubwa ya uhamasishaji iliyofanywa na waandaaji.
“Ni heshima kubwa kwetu kupata tuzo hii kwa mwaka wa pili mfululizo. Tunawashukuru viongozi wa TanTrade kwa kutupa heshima hii na kutuongezea hamasa ya kuendelea kuboresha huduma na bidhaa zetu,” alisema Karmali.
Alibainisha kuwa katika maonesho ya mwaka huu, GF Trucks and Equipment imewasilisha bidhaa mbalimbali ikiwemo magari madogo, malori, mitambo mizito pamoja na mashine za kisasa za utafiti na uchimbaji maji.
Kwa mujibu wake, kivutio kikubwa katika banda lao ni mitambo ya dozer pamoja na mashine za utafiti na uchimbaji zinazojulikana kama drilling rigs au exploration rigs, ambazo hutumika katika kufanya tafiti za vyanzo vya maji na shughuli nyingine za uchimbaji.
Karmali alisema baadhi ya mitambo hiyo imebuniwa kwa kuzingatia mahitaji ya mazingira ya Tanzania, baada ya kufanyiwa tafiti za kina ili kuhakikisha inafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.
Aidha, alisema kampuni hiyo inaendelea kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira kwa kuleta teknolojia zinazopunguza matumizi ya mafuta na kupunguza athari kwa mazingira.
“Kwa sasa dunia inaelekea kwenye matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira. Sisi tumekuja na bidhaa zenye matumizi madogo ya mafuta na pia tumewaletea magari yanayotumia umeme ya chapa ya Hyundai, ambayo tayari yameanza kutambulishwa nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa kampuni hiyo itaendelea kutoa ofa maalum kwa wateja wake hadi mwisho wa maonesho hayo na kuwataka wananchi pamoja na wadau wa sekta mbalimbali kutembelea banda lao ili kujionea teknolojia hizo mpya.

