NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imeeleza kuwa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamechangia kuzalishwa kwa ajira zaidi ya 631,109 katika kipindi cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, huku ajira nyingine zaidi ya 20,000 zikitarajiwa kupatikana katika maonesho ya mwaka huu.
Hayo yamebainishwa leo Julai 3,2015 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa TanTrade Dk. Latifa Khamis mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo yaliyoanza rasmi Juni 28 na yanatarajiwa kumalizika Julai 13, mwaka huu.
Dk. Khamis amesema mafanikio hayo yaliyopatikana yanaonyesha mchango mkubwa wa maonesho hayo katika kukuza biashara, uwekezaji na ustawi wa uchumi wa Taifa.
Amesema katika kipindi cha miaka 50, maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi, hatua iliyochochea ukuaji wa sekta mbalimbali za uchumi.
Dk. Khamis amefafanua kuwa katika kipindi hicho maonesho hayo yameshirikisha nchi 59 zikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, China na nyinginezo, huku yakivutia washiriki zaidi ya 38,000 na kutembelewa na watu zaidi ya milioni 74.
Aidha, amesema maonesho hayo yamewezesha kufanyika kwa mamia ya fursa za biashara na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ramani ya biashara ya kikanda na kimataifa.
Mkurugenzi huyo amesema matarajio ya maonesho ya mwaka huu ni kuvutia washiriki zaidi ya 4,800, watembeleaji zaidi ya 624,130 pamoja na kuwezesha biashara zaidi ya 352, sambamba na kuongeza mauzo ya papo kwa papo.
“Mafanikio haya ni tafsiri ya nafasi ya TanTrade kama taasisi inayochochea biashara, uwekezaji na ajira nchini. Tunaendelea kuimarisha mchango wetu katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya Taifa kupitia sekta ya biashara na diplomasia ya uchumi,” amesema na kuongeza
“TanTrade ni daraja linalounganisha sekta zote za uzalishaji na masoko ya ndani na nje ya nchi. Kupitia kampeni ya Tanzania Brand tunaendelea kuitangaza Tanzania na bidhaa zake katika soko la dunia,” amesema
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya East Africa Commercial and Logistics Center (EACLC), Catherine Wang, ambao ndio wadhamini Wakuu wa maonesho hayo ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na TanTrade kwa maandalizi mazuri ya Maonesho ya 50 ya DITF, akisema maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kukuza biashara, uwekezaji, ubunifu na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mbalimbali duniani.
Wang pia alimshukuru Rais Samia kwa uongozi wake na juhudi za kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
Aidha, alimkaribisha kwa heshima Rais Chapo, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, akieleza kuwa uwepo wake katika maonesho hayo ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Tanzania na Msumbiji.
Maonesho ya 50 ya Sabasaba yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Tanzania kwa lengo la kukuza biashara na fursa za uwekezaji.

