NA MWANDISHI WETU,BAGAMOYO,PWANI
MKUU wa Wilaya ya Bagamoyo Shaib Ndemanga ameipongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kuimarisha suala la kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na uhamasishaji wa matumizi ya pembejeo hiyo kwa wakulima na kuwezesha kuongeza tija ya uzalishaji.
Amesema, nguvu kubwa iliyowekwa katika kuwajengea uwezo wakulima hao na yeye akiwa miongoni mwao imechangia pia katika kuimarisha uchumi wa mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla na hivyo kupunguza umaskini.
Ndemanga ametoa pongezi hizo Machi 05,2026 alipokuwa akifungua kikao cha baraza la wafanyakazi wa Mamlaka hiyo kilichofanyika Bagamoyo mkoani Pwani.
“Tunalo jukumu la kuhakikisha wakulima wanatumia mbolea kwenye kilimo chao na sio tu kutumia mbolea bali kutumia mbolea kwa usahihi na TFRA mmelisimamia kikamilifu sana na tunaona mabadiliko kwenye jamii tunazozihudumia”. ameongeza.
Aidha, ametoa wito kwa Mamlaka kuongeza wigo wa mafunzo mpaka kwa wataalam wa kilimo ngazi za Kata na vijiji ili waweze kutoa elimu hiyo kwa wakulima wanaowahudumia kwa ufanisi zaidi pamoja na kufuatilia uendelevu wa matumizi ya mbolea kwa wakulima ili kuongeza tija.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Joel Laurent ameeleza kuwa, kikao hicho ni fursa ya kujadili mafanikio, changamoto na mikakati itakayotuwezesha kuzikabili changamoto zinazoikabili Mamlaka.
Aidha, ameeleza kuwa tangu kuanza kutekelezwa kwa Mpango wa Mbolea za ruzuku pamoja na uhamasishaji wa matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima nchini kumekuwa na ongezeko la matumizi ya mbolea kwa wakulima kutoka tani 580,628 mwaka 2022/23 hadi kufikia tani 972,506 msimu wa kilimo wa 2024/2025.
Amewataka Wajumbe wa baraza kushiriki kikamilifu katika mkutano na kueleza maoni yao yatachangia katika kukamilishaji wa maandalizi ya bajeti kwa mwaka 2026/2027 na uhuhishaji wa Strategic plan ya Mamlaka kunakotarajiwa sana na Menejimenti.
Naye Nsubisi Mwasandende Mwakilishi wa TUGHE kutoka Makao Makuu ya chama hicho cha wafanyakazi ameipongeza Mamlaka kwa namna wanavyoendesha vikao vyao kwa uwazi na amani na kukiri kuwa mwenendo huo umechangia kwa kiasi kikubwa ufanisi katika kuwahudumia wakulima.







