NA JANETH JOVIN, DAR ES SALAAM
MIAKA ya hivi karibuni wataalamu wa afya wamekuwa wakionya kuhusu ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza miongoni mwa watoto na vijana, hali inayotishia mustakabali wa kizazi kijacho.
Tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo magonjwa kama shinikizo la damu, matatizo ya moyo na mishipa ya damu yalionekana zaidi kwa watu wazima, sasa yameanza kuonekana mapema kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha na hasa ulaji wa vyakula visivyo na lishe bora.
Moja ya sababu kubwa inayochangia tatizo hilo ni matumizi ya vyakula vyenye Tran fat acid. Haya ni mafuta hatarishi yanayotengenezwa wakati mafuta ya kawaida yanapobadilishwa kemikali ili yadumu muda mrefu au yanapopashwa moto kwa joto kali sana, hasa wakati wa kukaanga mara kwa mara.
Mafuta haya hupatikana zaidi kwenye vyakula vilivyosindikwa viwandani kama biskuti, keki, chipsi, vyakula vya kukaanga haraka, pamoja na baadhi ya bidhaa za dukani zinazodumu muda mrefu bila kuharibika.
Hata hivyo Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa magonjwa yasiyoambukiza (NCD) yanachangia takribani asilimia 74 ya vifo vyote duniani, sawa na vifo zaidi ya milioni 41 kila mwaka.
Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba, zaidi ya watu milioni 15 hufariki dunia mapema wakiwa na umri kati ya miaka 30 hadi 69, hali inayoathiri nguvu kazi ya jamii na uchumi wa nchi nyingi, hususan zile zenye kipato cha chini na cha kati, ikiwemo Tanzania.
Kwa mujibu wa WHO, wameonya kuwa endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, vifo vinavyotokana na matumizi ya mafuta hayo ya Trans Fatty Acids vinaweza kuongezeka hadi milioni tani duniani kufika 2030.
Daktari Hassan Lusobya, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), anabainisha kuwa ongezeko la uzito kwa watoto na vijana pamoja na kuibuka kwa magonjwa yasiyoambukiza linahusishwa kwa kiasi kikubwa na vyakula wanavyokula kila siku.
Anasema changamoto hiyo inachangiwa na tabia ya kula vyakula vilivyosindikwa viwandani ambavyo vina kiwango kikubwa cha mafuta, chumvi na sukari.
Kwa mujibu wa Dk. Lusobya, siku hizi watu wengi hawapiki nyumbani mara kwa mara bali hula kazini au shuleni, hali inayowafanya watoto kula vyakula ambavyo hawajui vimetayarishwaje.
Aidha, vyakula vingi hununuliwa kwenye maduka makubwa bila wazazi kufuatilia taarifa za lishe zilizopo kwenye vifungashio. Anatahadharisha kuwa hali hiyo imechangia kuongezeka kwa matatizo ya moyo, presha na maradhi ya mishipa ya damu hata kwa vijana wadogo.
Anasema hali hiyo imechangia kuongezeka kwa matatizo ya moyo, presha na magonjwa ya mishipa ya damu hata kwa umri mdogo. Kwa mujibu wake, hatua muhimu ya kujikinga ni kusoma taarifa za lishe kwenye lebo za bidhaa kabla ya kununua.
“Changamoto kubwa inatokana na vyakula vilivyosindikwa ambavyo vina mafuta, chumvi na sukari nyingi. Watoto wengi siku hizi hawali chakula cha nyumbani mara kwa mara, wanakula shuleni au kununua dukani bila kujua vimetayarishwaje,” anafafanua.
Anasisitiza kuwa hatua muhimu ya kujikinga ni kusoma lebo ya lishe kwenye bidhaa kabla ya kuinunua. Taarifa hiyo humwezesha mnunuzi kujua bidhaa imetengenezwa na nini pamoja na kiwango cha mafuta ya Trans fatty Acids, chumvi na sukari.
Anasema ikiwa bidhaa ina zaidi ya asilimia moja au gramu moja hadi mbili za Trans fatty Acids, kiwango hicho kinachukuliwa kuwa kikubwa na si salama kwa afya, hasa kwa mtu anayetaka kuepuka uzito uliopitiliza na magonjwa ya moyo.
“Mafuta haya ya Trans Fatty Acids yanaharibu mfumo wa hooni na huongeza lehemu mbaya (LDL) kisha ushusha lehemu nzuri (HDL) hali hiyo inaongeza hatari ya kupata maradhi ya moyo hata kwa watoto na vijana,” anasema
Dk. Lusobya anashauri wazazi kuzingatia maandalizi ya chakula cha nyumbani kwa watoto wao badala ya kutegemea vyakula vya shuleni au vya kununua njiani ambavyo mara nyingi huwa na chumvi na sukari nyingi.
Anawaonya pia watengenezaji wa vyakula vya kukaanga, hususan chipsi, kuacha kutumia mafuta yale yale mara nyingi kwa sababu kuyapasha moto mara kwa mara huongeza uwezekano wa kutengeneza Trans fatty Acids hatarishi.
Mbali na wataalamu, wazazi nao wameanza kugundua hatari inayowakabili watoto wao. Rehema Msuya, mzazi mkazi wa Dar es Salaam, anasema awali alikuwa akiwapa watoto wake fedha za kununua vitafunwa shuleni bila kufuatilia wanachokula.
“Nilipogundua mtoto wangu ameanza kunenepa kupita kiasi, daktari alinieleza tatizo linaweza kuwa vyakula vya dukani. Sasa nawaandalia chakula cha nyumbani na naona mabadiliko,” anasema.
Naye John Mwakalinga, mzazi wa mwanafunzi wa sekondari, anasema changamoto ni upatikanaji rahisi wa vyakula visivyo na afya karibu na shule.
“Watoto wanavutiwa na chipsi na vitafunwa vyenye mafuta mengi. Hata ukiwazuia nyumbani, nje wanapata kirahisi. Elimu kwa wazazi na watoto ni muhimu,” anasisitiza.
Wataalamu wa lishe wanakubaliana na hoja hiyo na kusisitiza kuwa wazazi wana jukumu kubwa la kusimamia mlo wa watoto tangu wakiwa wadogo huku wakisisitiza kuwa lishe bora si lazima iwe ghali bali ni suala la uchaguzi sahihi wa vyakula.
“Chakula cha asili kama matunda, mboga za majani, nafaka zisizokobolewa na protini za asili kinasaidia kulinda afya ya mtoto. Tatizo ni utegemezi wa vyakula vya viwandani ambavyo vina vihifadhi na mafuta yasiyofaa,” wanasema wataalamu hao
Kwa upande wa udhibiti, Dk. Lusobya anabainisha kuwa Tanzania bado haina sheria maalumu inayowalazimisha wakaguzi kupima kiwango cha Trans fatty Acids kwenye bidhaa za chakula.
Anasema kutokuwepo kwa sheria hiyo kunafanya bidhaa nyingi kuingia sokoni bila kudhibitiwa kiwango cha mafuta hayo. Anaamini kuwa kuwepo kwa sheria kutawapa mamlaka kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) uwezo wa kupima na kudhibiti viwango hivyo, hatua itakayosaidia kupunguza hatari kwa watumiaji.
Kwa ujumla, wataalamu wanasisitiza kuwa mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza yanapaswa kuanzia utotoni kwa kuhimiza lishe bora, kupunguza vyakula vilivyosindikwa, na kuongeza uelewa wa kusoma taarifa za lishe.
Ni wazi kuwa bila hatua hizo, ongezeko la magonjwa hayo kwa watoto na vijana linaweza kugeuka kuwa janga la afya ya jamii katika miaka ijayo.


