NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR
TAASISI za kifedha na kampuni mbalimbali zimetakiwa kujitoa kikamilifu katika kusaidia shughuli za kijamii, ikiwemo kutenga sehemu ya faida wanazopata kwa ajili ya kusaidia jamii zinazowazunguka katika maeneo wanayofanya biashara.
Wito huo umetolewa sambamba na kukumbushwa kuwa usafi ni jukumu la kila mtu, huku Benki ya Biashara ya KCB ikitajwa kama mfano wa kuigwa baada ya kuamua kuunga mkono jitihada za Serikali ya Zanzibar katika kudumisha usafi na utunzaji wa mazingira, ikitambua kuwa usafi ni afya.
Katika kuonesha dhamira hiyo, KCB imefanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Soko la Darajani, Manispaa ya Mjini Zanzibar, hatua iliyolenga kutoa hamasa kwa wananchi na wafanyabiashara kuendeleza utamaduni wa usafi katika maeneo yao ya biashara.
Akizungumza kuhusu mchango huo, Mkuu wa Soko la Darajani, Mariam Juma Mzee, amesema hatua ya KCB imewapa faraja kubwa, akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo kwa kuunga mkono juhudi za kudumisha usafi katika masoko ili kuhakikisha afya bora kwa wafanyabiashara na watumiaji wa soko hilo.
“Tunazishukuru sana taasisi kama KCB kwa kuunga mkono usafi sokoni. Hii inasaidia kuimarisha afya na mazingira bora kwa wote,” amesema Mariam Juma Mzee.
Kwa upande wao, baadhi ya wafanyabiashara katika Soko la Darajani wamesema shughuli hizo za usafi zina umuhimu mkubwa, wakieleza kuwa mazingira safi huongeza mvuto wa wateja na kupunguza hatari ya magonjwa.
Kupitia hatua hiyo, KCB imeendelea kuonesha dhamira yake ya kushiriki katika maendeleo ya jamii kwa vitendo, hususan katika nyanja ya afya na uhifadhi wa mazingira.






