NA MWANDISHI WETU, MSALALA,SHINYANGA
WANANCHI wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka Mgodi wa dhahabu wa Barrick Bulyanhulu uliopo Msalala mkoani Shinyanga, wameushukuru mgodi huo kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kijamii ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, shule na miundombinu mingine muhimu kwa ustawi wa jamii.
Wakizungumza wakati wa maadhimisho ya ‘Family Day 2025’ yaliyoandaliwa na mgodi huo, wananchi hao wamesema ushirikiano uliopo kati yao na Barrick Bulyanhulu umeleta mabadiliko chanya katika maisha yao na kuimarisha mahusiano mema kati ya mgodi na jamii inayouzunguka.
Mkazi wa kijiji cha Bugarama, John Mhando, amesema Barrick Bulyanhulu imekuwa bega kwa bega na wananchi katika kutatua changamoto za kijamii.
“Kupitia mgodi huu tumepata shule, vituo vya afya na msaada katika miundombinu mbalimbali hii inaonesha kuwa Barrick Bulyanhulu si mgodi tu bali ni mdau wa kweli wa maendeleo ya jamii,” Mhando.
Akielezea furaha yake, Rehema Shija, mkazi wa kijiji jirani na mgodi huo, amesema hafla ya Family Day imewapa fursa ya kuungana na wafanyakazi wa mgodi huo na kujiona kuwa sehemu ya familia moja.
“Tunaishi vizuri na mgodi, wanatusikiliza na wanachangia maendeleo yetu tunawashukuru kwa kutuandalia siku hii ambayo imetuletea furaha na umoja,” almesema Shija.
Akizungumza katika hafla hiyo, Kaimu Meneja wa Mgodi wa Barrick Bulyanhulu, Leon Ebondo, amewashukuru wananchi na wageni wote waliohudhuria, akisisitiza kuwa mgodi huo utaendelea kushirikiana na jamii inayouzunguka katika kuchochea maendeleo endelevu.
“Tunathamini sana ushirikiano wetu na jamii. Family Day ni sehemu ya kuimarisha mshikamano na kuhakikisha wananchi wanajiona kuwa sehemu ya mafanikio ya mgodi,” amesema Ebondo.
Hafla hiyo imeendelea kuonesha dhamira ya Barrick Bulyanhulu ya kujenga mahusiano ya kudumu na jamii inayouzunguka, sambamba na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Mkoa wa Shinyanga.






