NA JANETH JOVIN,DAR ES SALAAM
MKUU wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Dk. Prosper Mgaya amesema kuwa ufanisi wa wafanyakazi wa chuo hicho una uhusiano wa moja kwa moja na afya zao, hivyo kuanzishwa kwa bonanza la michezo ni hatua muhimu katika kuimarisha ustawi wa watumishi pamoja na kuongeza tija katika utendaji kazi.
Akizungumza wakati wa kilele cha Bonanza la Michezo la Watumishi wa NIT, lililoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho cha NIT, Dk. Mgaya amesema bonanza hilo lilianza mwaka jana na limehusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, peke, kuvuta kamba, karata na bao.
Ameeleza kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa bonanza hilo ni kuwahamasisha wafanyakazi kupenda na kushiriki michezo kama njia ya kuboresha afya zao, kujenga mshikamano, kuimarisha mahusiano kazini pamoja na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Michezo ni afya, na afya njema ndiyo msingi wa ufanisi kazini. Kupitia bonanza hili tunalenga kuhamasisha wafanyakazi wetu kushiriki kikamilifu katika michezo ili kuwa na nguvu, ari na utayari wa kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” amesema
Mkuu huyo wa NIT ameongeza kuwa Bonanza hilo litakuwa endelevu na chuo kitatenga siku maalum kwa ajili ya wafanyakazi kufanya mazoezi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kudumisha afya na ustawi wao kwa muda mrefu.
Aidha, ametoa rai kwa wafanyakazi wote 550 wa NIT kujitokeza kwa wingi kushiriki katika michezo hiyo kwa lengo la kuimarisha afya zao, kuongeza mshikamano na hatimaye kuinua kiwango cha utendaji kazi ndani ya chuo.
Hata hivyo Dk. Mgaya amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza kudhamini bonaza hilo wakiwemo Benki ya NMB, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Kwa upande wake, Katibu wa Maandalizi ya Bonanza hilo, Getrude Challe, amesema wamefanikiwa kuandaa bonanza hilo kwa mafanikio makubwa ambapo washindi wamepatikana katika michezo mbalimbali.
Ameeleza kuwa ushiriki wa wafanyakazi umekuwa mzuri na amewasihi kuendelea kushiriki kikamilifu katika michezo hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuipa michezo kipaumbele kama njia ya kuboresha afya zao na kuwa kamili katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.
Naye Kapteni wa washindi wa jumla wa bonanza hilo, Cornelio Swai, ameushukuru uongozi wa NIT pamoja na waandaaji wa bonanza hilo kwa kuweka mazingira rafiki yanayowahamasisha wafanyakazi kufanya mazoezi, kujuana, kujenga mshikamano na kuimarisha mahusiano kazini.
Amesema bonanza hilo limekuwa chachu muhimu ya kuleta umoja, afya njema na mshikamano miongoni mwa wafanyakazi wa NIT.






